
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli leo Alhamisi, Juni 1, 2017 amezindua rasmi Mfumo wa Serikali wa Ukusanyaji Mapato kwa njia ya Kielektroniki.

Katika uzinduzi huo uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa ngazi za juu wa serikali wakiwemo Rais wa Zanzibar, Dkt. Ally Mohammed Shein, Makamu wa Rais, Bi. Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa na wengine, Rais Magufuli alianza kukagua Kituo cha Taifa cha Kutunzia Taarifa (Data Center), kilichopo TTCL Kijitonyama na kuridhishwa na mafanikio makubwa ya ubunifu huo.

“Nimetembelea Kituo cha Taifa cha Kutunzia Taarifa (Data Center), nimeridhika na nimefurahi kuona mafanikio makubwa kwa nchi yetu hasa katika sekta ya teknolojia.
“Sababu za kuazisha Data Center ni pamoja na kuhifadhi data kwa usalama na kukuza sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano.

“Tangu serikali ilipobinafsisha Kampuni ya TTCL mwaka 1992 haikuwahi kupata gawio la faida hata moja wakati kipindi hatujabinafsisha tulikuwa tunapata gawio la zaidi ya bilioni moja. Tuliamua kuichukua tena TTCL baada ya kuona haitengenezi faida, ila tangu tumeichukua imeanza kufanya vizuri” alisema Magufuli.
Wakati huo Rais Magufuli ameiagiza TCRA, kutoyapiga faini makampuni ya simu ambayo hayajajiorodhesha kwenye Soko la Hisa la Dar (DSE), badala yake wayafute kabisa ambapo tangu serikali itangaze ni Kampuni ya Vodacom pekee ndiyo imejisajili.

“Tulitangaza makampuni ya simu yajiunge na DSE na yamejizungusha na ni Vodacom pekee walijiunga. Makampuni ya simu kama mnajiamini kuwa mnalipa kodi, mnaogopa nini kujiunga na DSE tuone mapato yenu? TCRA, makampuni ya simu ambayo hayajajiorodhesha DSE msiyapige faini, yafuteni. Ni lazima tutoe maamuzi hata kama yanauma,” alisisitiza Rais Magufuli.
Rais ameyataka makampuni ya simu na mabenki kujisajili kwenye mfumo huo ili kurahisisha ukusanyaji wa kodi za serikali kwa uharaka na uaminifu zaidi.

Pia amesema kwa kuwa sasa kuna Kituo cha Taifa cha Kutunzia Taarifa, hivyo wizara na idara zote zisijenge tena data center nyingine badala yake zitumie hiyo ya taifa kwani kujenga nyingine ni gharama kubwa.
“Kituo hiki kitasaidia kupunguza kero za muungano kwani mtu akinunua vocha akiwa Zanzibar, kodi itakwenda Zanzibar. Kwa vile tuna Kituo cha Kuhifadhi Kumbukumbu cha Taifa, sitaki kuona wizara nyingine au idara inajenga kituo chake cha kumbukumbu,” alisema Rais Magufuli.
Baada ya hapo Rais Magufuli alizindua rasmi Mfumo wa Serikali wa Ukusanyaji wa Mapato Kielektroniki ambapo alielekezwa namna ambavyo mfumo huo unavyofanya kazi.
Rais Magufuli, Makamu wa Rais, Bi. Samia Suluhu na Rais wa Zanzibar, Dk. Ally Mohammed Shein walikabidhiwa iPads za kuwawezesha kuona mapato ya serikali yaliyokusanywa na mfumo huo wa kielektroniki.