
Na Saleh Ally
TANZANIA imepata ugeni wa wadau wa soka ambao inawezekana kila kiongozi au mchezaji angependa kujifunza kupitia kwao.
Hao ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Everton ya England, Robert Elstone pamoja na mchezaji gwiji wa klabu hiyo, Leon Osman, mmoja wa viungo waliocheza mechi nyingi zaidi wakiwa na Everton.
Osman amecheza mechi 400 akiwa na kikosi cha Everton na yeye pamoja na bosi wake, walikuwa Tanzania kwa siku mbili katika mkutano wao na uongozi wa SportPesa Tanzania.
SportPesa sasa ndiyo wadhamini wakuu wa Everton ambayo msimu uliopita ilimaliza katika nafasi ya saba nyuma ya Manchester United na Elstone anaamini wanaweza kujipanga zaidi.
Everton itakuwa nchini Julai 13, kucheza na bingwa wa SportPesa Super Cup ambaye atapatikana baada ya michuano itakayoshirikisha timu za Kenya na Tanzania.
Mahojiano maalum kupitia Global TV Online pamoja na Elstone, baada ya hapo alifuatia Osman ambaye alizungumzia mambo kadhaa ikiwemo kuhusiana na wachezaji Waafrika anaowakubali zaidi.
Mahojiano hayo hayakuwa marefu kwa kuwa walitakiwa kuondoka kuwahi ndege kwa kuwa wanarejea England.

Everton imewahi kubeba makombe tisa ya Ligi Kuu England, matano ya Kombe la FA pia ubingwa wa Ulaya mara moja lakini imekuwa ikipata shida kubeba ubingwa tena. Mara ya mwisho ubingwa England ilikuwa msimu wa 1986-87.
Everton imecheza jumla ya misimu 114 katika ligi ikiwa ni mingi zaidi ya klabu yoyote ile na imecheza misimu 63 mfululizo bila ya kuteremka daraja ligi kuu.