The House of Favourite Newspapers

Mungu Ndiye Hupanga Muda wa Wewe Kupata Mtoto-2

0

Na Gabriel Ng’osha | IJUMAA WIKIENDA | XX Love

KWA wenzetu Waislam leo ni chungu cha kumi na moja kwenye Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Safu hii inawatakia kila la kheri kwenye kipindi hiki cha nguzo ya nne ya Dini ya Kiislam.

Nikukaribishe mpenzi msomaji wa safu hii kwenye sehemu ya pili ya mada tajwa hapo juu. Wiki iliyopita nilizungumza mambo mengi ambayo wamekuwa wakikutananayo wanawake ambao hawajabahatika kupata watoto.

Suala la mtoto limekuwa likizifanya ndoa nyingi kuingia kwenye mifarakano ya mara kwa mara kwa sababu tu haina mtoto au watoto. Mzazi wa mwanamke au mwanaume anahitaji mtoto, lakini katika uhalisia, pengine muda wa Mungu kuwazawadia zawadi hiyo kwenye ndoa yao haujafika.

Kinachoumiza ni kitendo cha baadhi ya wanaume na ndugu kuwabebesha lawama wanawake walioolewa na ndugu zao. Eti unakuta wifi anamsengenya mke wa kaka yake, mama mkwe naye anamnyali mke wa mtoto wake, ukiuliza, kisa unaambiwa “ndugu zake wanataka mtoto, yule mwanamke hana uzazi”. Kiukweli wanawake ambao hawajapata watoto huwa wanapitia mambo mengi kwenye uhusiano wao.

Kwa mwanaume mwenye upendo wa dhati kwa mwenza wake, hana sababu ya kumchukia mke kwa sababu hana mtoto au hajapata ujauzito. Kwanza anaanzaje kumuhukumu wakati yeye mwenyewe hana uhakika kama ni msafi kiasi cha kuhukumu?

Hata vitabu vitakatifu vinakataza kuhukumu kwani nawe utahukumiwa. Suala la kumlamu mwenza wako kutopata mtoto haliko kwenye uwezo wa kibinadamu.

Labda kama kuna sababu za kibinadamu ambazo pia inawezekana ni za bahati mbaya au kutokuelewa.

Naamini katika kumpenda na kumchagua kwako, ulikubali kuishi naye kwenye shida na raha, sasa inakuwaje kwenye tatizo hilo unataka kumuacha peke yake? Kwa nini unataka kumuongeza mwanamke mwingine kwa sababu uliyenaye hashiki mimba?

Hivi utajisikiaje kama mwenza wako siku moja akikukimbia kwa sababu tu umeishiwa ‘mpunga’? Bila shaka hutafurahia. Kama ndivyo, basi usimuhukumu kwa yeye kutokushika mimba badala yake mfarijiane katika kipindi hicho kigumu. Hata yeye mwenyewe anapenda kuwa na mtoto lakini hana uwezo wa kujitungisha mimba.

Wanawake wengine wanadiriki kuamua kuiba watoto hospitalini au kwenda kwa waganga ili wapewe dawa ya kupata watoto ili wawaridhishe waume zao, mawifi, mama au baba wakwe ambao wamekuwa wakiwatusi kuwa wanakula chakula cha bure cha ndugu yao na kujaza choo.

Maneno hayo yanauma, kumnyong’onyesha na kumuathiri kisaikolojia mwanamke.

Wanawake wanatukanwa matusi ya ajabu kwa sababu ya kukosa mtoto, wengine wanaingia mikononi mwa sheria na kufungwa kisa kikiwa kuiba mtoto. Uchungu wa mwanamke anayefungwa kwa ajili ya kukosa mtoto utakuwa wa maumivu makali.

Wanaume wengi mmekuwa mkiwalaumu wanawake kuwa ndiyo chanzo cha kushindwa kupata watoto wakati si kweli.

Kama mumeishi muda mrefu bila kupata mtoto nendeni hospitali mkapimwe huku mkimuomba Mungu.

Mpenzi msomaji, kwa ushauri na maoni, tembelea ukurasa wetu wa Gazeti la Ijumaa Wikienda, Insta:@mimi_na_ uhusiano au jiunge na M&U WhatsApp kwa namba zilizopo hapo juu.

Leave A Reply