
NA GABRIEL NG’OSHA +255 620 744 592| Risasi Mchanganyiko | Barua Nzito
Kwanza kabisa napenda kuwatakia mfungo mwema wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ndugu zangu Waislam wote duniani kwa sababu wanatimiza wajibu wa imani yao. Huu ni mwezi wa kujitathmini kwa wanayofanya ili kurekebisha mapito yao. Kama kawaida, nimekuwa nikiandika barua hii kwa ajili ya kukumbushana palipo na tatizo au changamoto na leo naielekeza kwa wasanii mastaa wa fani zote hususan Bongo Muvi na Bongo Fleva.
Kipindi hiki cha mfungo ni sawa na Wakristo wanavyopitia msimu wa Kwaresma, ambapo hufunga kwa kukumbuka mateso ya Bwana Yesu Kristo. Ni mwezi wa kuomba toba na msamaha ili siku Mwenyezi Mungu anapokuita katika ufalme wake, apate kukuweka sehemu salama. Mungu ni mwema, anajua wanadamu tu wadhaifu, anafahamu hatuwezi kujizuia siku zote ndiyo maana ukawepo muda huu maalum kwa watu wa imani zote, wapate kutubu madhambi yao pamoja na kuomba toba.

Nilichojifunza mwezi huu, wengi wetu huwa na utu, wanakuwa waungwana, wenye unyenyekevu, wenye kutenda yaliyo mema na kupenda wenzao. Ndicho kipindi utawaona watu wakifuturisha, wakitembelea vituo vya watoto yatima, wagonjwa, wakitoa zawadi kwa wasiyojiweza na mambo mengine kadha wa kadha mema, jambo ambalo ni zuri na la msingi. Wanaofanya haya ni wengi na miongoni mwao, wapo kaka na dada zangu kutoka Bongo Muvi na Bongo Fleva.
Kuna maswali mengi ya kujiuliza juu yao, lakini kitu kikubwa ambacho leo ningependa niseme nao, ni juu ya mwezi huu kuwa wa somo la kudumu. Kama mtu anaweza kujisitiri kwa kuvaa mavazi mazuri yenye heshima mbele za watu, kama anaweza akawa na lugha nzuri kwa wanaomzunguka, akawa na moyo wa huruma, wenye kujali walio na mahitaji, kwa nini jambo hili liwe la mpito na siyo la kudumu? Sioni kama ni vyema kutenda mambo mazuri kama kutoa sadaka au misaada kwa wahitaji hadi ifike Ramadhani. Kama lengo ni kumtendea Mungu yaliyo mema, hii siyo sawa, lakini kama lengo ni kutafuta ‘coverage’ ya media basi ni sawa.

Katika mitandao ya kijamii, wasanii wengi wanatupia picha zenye kuashiria uadilifu wao kwa jamii, kama ni akina dada wakiwa wamevaa vizuri mavazi yenye heshima, yenye kufunika sehemu kubwa ya miili yao, kama ambavyo unaona kwa kaka zao, nao wakiwa wametupia mavazi ya heshima, tena wakionekana wamewabeba watoto kwa furaha . Unapotazama jambo hili, unaona wazi kuwa kumbe jambo hili linawezekana, kwamba wale dada zangu wanaweza kabisa kuendelea na shughuli zao za kisanii wakiwa wamevaa vyema, wakibaki na heshima yao kubwa kuliko vile ambavyo jamii inaelekea kuwazoea.

Kwamba wanaweza kutupia clip za video katika akaunti zao wakiwa wanawafundisha watoto tabia njema, badala ya zile za kuonyesha nusu utupu na wakati mwingine wakitingisha makalio yao kama vile wanawaalika wakware wawafuate.
Kumbe hata wale kaka zangu nao, wanaweza kuwa mifano bora kwa wadogo zao huko majumbani, wakaacha kutuvalia ile milegezo yao, wakaacha mbwembwe zao za kushindana na dada zao katika kusuka nywele na kutoboa pua na masikio. Ushauri wangu kwao, msitende mambo ya kumpendeza Mungu na jamii kwa jumla kwa mwezi mmoja tu, bali fanye hii iwe sehemu ya maisha yenu, acheni kujifanya watakatifu wakati wa mfungo na ukiisha mnaendeleza mambo yenu yasiyopendeza.