
STORI NA WAANDISHI WETU | RISASI JUMAMOSI | MPAKA HOME
MAMBO vipi mpenzi msomaji wa safu hii ya Mpaka Home, kama ilivyo kawaida ya kila Jumamosi huwa tunakuletea mastaa mbalimbali ambao wanaonesha maisha yao ya nyumbani wakiwa nje ya kazi zao. Wiki hii Mpaka Home ilimtembelea msanii mkongwe wa filamu ambaye kwa sasa ni mshehereshaji (MC) maarufu Bongo, Gladys Chiduo ‘Zipompa’ anayeishi maeneo ya Big Brother, Dar ambaye ana mengi ya kueleza nje ya kazi yake ya u-mc ungana naye hapa.

Mpaka Home: Hongera kwa kuwa na nyumbanyumba nzuri. Zipompa: Asante.
Mpaka Home: Hapa nyumbani kwako unaishi na nani?
Zipompa: Naishi na familia yangu yaani mama yangu, dada yangu na mjukuu wangu.

Mpaka Home: Ni kitu gani hasa unapenda kukifanya ukiwa nyumbani?
Zipompa: Napenda sana kulala na kuchati na marafiki zangu huo ndiyo ugonjwa wangu.
Mpaka Home: Huwa unapika au unapikiwa? Zipompa: Ninapika siku nikijisikia na napenda sana kupika rosti na chapati ila niandaliwe kila kitu kazi yangu iwe ni kuvichanganya tu, siku nyingine anapika dada.

Mpaka Home: Ratiba yako kwa siku ikoje? Zipompa: Nikiamka asubuhi nafanya usafi chooni kwangu, chumbani, natandika kitanda, naoga, navaa kisha naondoka zangu.
Mpaka Home: Kwenye ratiba yako hujataja kifungua kinywa, hunywi chai asubuhi?
Zipompa: Asubuhi huwa sipendi kula chochote nakunywa maji ya moto tu mpaka mchana ndiyo nakula.

Mpaka Home: Vipi kuhusiana na kazi za nyumbani anakufanyia nani?
Zipompa: Nina dada wa kazi ndiye anayenifanyia kazi ikiwa ni pamoja na kunifulia nguo. Mpaka Home: Unene wako unatokana na kula au ni nini?

Zipompa: Nilizaliwa hivi na ukoo wetu wote ni wanene. Mpaka Home: Siyo kama kula kunachangia maana naona unapenda mirostirosti?
Zipompa: Kula napenda na kunywa pia lakini kula siyo kunenepa jamani! Mpaka Home: Sasa ukiwa na kazi za usiku huwa unakula hukohuko au inakuwaje?

Zipompa: Huwa sili kwenye shughuli kabisa kwa sababu naogopa kuharibu kazi maana unaweza kula chakula ukaanza kuhara si nitaharibu kazi ya watu.
Mpaka Home: Kwa hiyo huwa unafanyaje?

Zipompa: Hata nikifika saa nane za usiku nyumbani huwa napasha chakula nakula au kwenye shughuli nafunga nyamanyama nakuja kula nyumbani baada ya kazi.

Mpaka Home: Nashukuru kwa ushirikiano.
Zipompa: Ahsante, karibu tena.