×

Hammer Q Akwaa Skendo ya Mwanaye

Msanii maarufu wa Muziki wa Kizazi Kipya nchini, Hussein Mohammed ‘Hammer Q’.

STORI: WAANDISHI WETU | RISASI JUMATANO | HABARI

DAR ES SALAAM: Msanii maarufu wa Muziki wa Kizazi Kipya nchini, Hussein Mohammed ‘Hammer Q’ amekwaa skendo ya kumtelekeza mtoto wake mwenyewe, aitwaye Faisal aliyezaa na mrembo Amina Said mwenyeji wa Zanzibar, Risasi Mchanganyiko limeambiwa.

Akisimulia kisanga hicho kwa masikitiko, mrembo huyo alisema alikutana kwa mara ya kwanza na Hammer Q miaka 14 iliyopita na kuanzisha uhusiano wa kimapenzi kabla ya kunasa ujauzito na kujifungua mtoto Feisal Hussein.

“Lakini hata kabla ya kujifungua, familia yangu ilinisusa kutokana na kubeba ujauzito wa mwanamuziki huyo. Mimi nilivumilia kwa sababu tu nilikuwa ninampenda, hata hivyo baada ya kujifungua, Hammer alinigeuka na kuacha kunihudumia.

“Wakati huo nilikuwa naishi Magomeni kwa dada aitwaye Hawa ambaye yeye alinitambulisha kuwa ni ndugu yake, sasa baada ya kuacha kunipa huduma ilinibidi nirudi nyumbani kwetu Zanzibar kuwaomba msamaha wazazi wangu ili wanihudumie mimi na mtoto wangu,” alisema Amina.

Alisema baada ya kufika Zenji na kusamehewa, bado aliendelea kumtafuta mzazi mwenziye lakini aliambulia kejeli na matusi, akiambiwa hahitajiki tena. Bila kujali, Amina anasema alimchukua kijana wake na kumpeleka nyumbani kwao Hammer ambako baadaye alimchukua na kwenda kuishi naye kwake Kimara.

“Baada ya Hammer kumchukua, baadaye nilipata taarifa kutoka kwa majirani wa pale nyumbani alipokuwa anaishi kuwa mwanangu alikuwa anaishi katika mazingira mabovu, alikuwa akiachwa peke yake hadi usiku.

“Niliamua kwenda kumchukua lakini hali niliyomkuta nayo ilikuwa inasikitisha mno. Alikuwa amekonda kuliko kawaida. Lakini pia ingawa ilikuwa ni miezi minne imepita tangu aende nyumbani hapo kwa baba yake lakini nguo alizoondoka nazo kwangu hazikuwa zimeongezeka hata kidogo,” alisema Amina.

“Mwanangu Feisal anaumwa. Yaani alipatwa na tatizo ambalo linamtokea kila anapopata mshituko wa ghafla. Yaani hapa mtu akiwasha redio ghafla, au watu wakipigana yeye hudondoka kama mtu mwenye kifafa.

“Tumehangaika sana mahospitalini na kwenye huduma mbalimbali za afya, lakini hatujaweza kufanikiwa kwa lolote zaidi ya kushauriwa kuwa tujihadhari mtoto asipate mshituko mkubwa,” alisema Amina.

Mwanadada huyo alisema hana lengo la kutaka kuishi na Hammer Q, ila anamtaka atoe msaada kwa mwanaye kwa sababu yeye hajiwezi na baba yake mzazi ambaye ndiye alikuwa akimtegemea, amekwishafariki dunia.

Akijibu tuhuma hizo, Hammer Q alikiri kumfahamu Amina, ni mama wa mtoto wake lakini walishindwa kuwa pamoja kutokana na tabia zake za kuhusishwa na masuala ya utapeli.

“Huyo mwanamke ninamfahamu. Ni mama wa mtoto wangu wa kwanza aitwaye Faisal. Madai yake kwamba nimemtelekeza mtoto wangu si ya kweli maana ingawa siwasiliani naye yeye, ninawasiliana na mama yake ambaye ni bibi wa mtoto wangu.

“Lakini pia mtoto huyo nimewahi kuishi naye, alishindwa kwenda shule kutokana na kukosekana cheti cha kuzaliwa. Nilijitahidi sana alete cheti cha kuzaliwa lakini hakufanya hivyo mpaka nilipomrudishia mtoto. Hata hivyo, yeye kama ameshindwa kumlea amlete kwangu muda wowote mimi nitamlea kwa sababu ni mtoto wangu. Lakini anatakiwa akija aje na cheti cha mtoto cha kuzaliwa,” alisema Hammer Q.

Leave a Comment