×

Denti UDSM Aliyeuawa na Polisi kwa Ujambazi Hatimaye Kuzikwa Kesho

Ndugu wa marehemu na viongozi wa dini wakizungumza na wanahabari

 

HATIMAYE mwili wa denti wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Salum Almas aliyeuawa kwa kupigwa risasi na polisi, Mei 14, mwaka huu maeneo ya Uhamiaji Kurasini jijini Dar es Salaam unatarajiwa kuzikwa kesho (Ijumaa) huku ndugu wakieleza sababu za kuamua hivyo.

 

Akizungumzia juu ya mazishi hayo baada ya kuususia mwili wa marehemu kwa zaidi ya siku 40, mjomba wa marehemu aliyefahamika kwa jina la Tullehya Abdulrahman alisema kuwa wamefi kia hatua hiyo baada ya kuona jitihada walizofanya juu ya kuionyesha jamii ukweli kuwa Almas hakuwa jambazi zimeanza kuzaa matunda.

 

“Ingawa Jeshi la Polisi lilitangaza kuwa Almas ni jambazi, sisi tunaamini siyo kweli. Almas alikuwa ni kijana mwema na mwenye mchango mkubwa tu kwenye jamii.

 

“Baada ya tukio hili kutokea tumepaza sana sauti ili kuweza kuionyesha jamii kuwa ndugu yetu hakuwa jambazi, tunamshukuru Mungu waandishi wa habari, taasisi za kutetea haki za binadamu na watu mbalimbali wametusaidia na wanaendelea kutusaidia juu ya hili na sasa tunakwenda kufanya mazishi tukiwa tunaamini ukweli unakwenda kufahamika,” alisema Tullehya.

 

Mjomba huyo aliongeza kuwa mbali na kuona mafanikio hayo ya ukweli wa Almas kutokuwa jambazi, wamekwenda mahakamani na kufungua kesi ya kudai haki ya marehemu kusingiziwa tukio la ujambazi.

 

“Kama nilivyosema awali mambo yanakwenda vizuri na Mungu akisaidia kesi yetu tuliyofungua mahakamani ikienda sawa ukweli zaidi juu ya kilichompata Almas utawekwa wazi.

 

“Hata hivyo, mengi zaidi tutayaanika siku ya mazishi pale kwenye Msikiti wa Kichangani, Magomeni ambapo ndipo tutakapomsomea marehemu dua kabla ya mazishi baada ya maiti kukaa mochwari ya Hospitali ya Muhimbili kwa takriban siku 48,” alisema Tullehya.

 

Mwili wa Almas uligomewa kuzikwa na ndugu zake kwa madai kuwa aliuawa kimakosa kwa kudhaniwa ni jambazi aliyetaka kupora fedha kwenye ATM iliyopo kwenye benki moja maeneo ya Uhamiaji, Kurasini jijini Dar.

 

STORI: BONIPHACE NGUMIJE NA GABRIEL NG’OSHA, DAR

Leave a Comment