
KWA siku mbili mfulululizo, baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Marian Girls iliyoko Bagamoyo Mkoani Pwani, wamefika katika Ofisi za Magazeti ya Global Publishers kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali juu namna kazi za kukusanya na kuandika habari zinafanyika, ikiwa ni pamoja na mchango wa tasnia hiyo kwenye jamii.

Katika kufanikisha hilo, wanafunzi hao walipata fursa ya kuhudhuria moja ya vikao vya uboreshaji wa magazeti hayo, ambayo ni Uwazi, Ijumaa, Amani, Risasi, Ijumaa Wikienda, Risasi Jumamosi, Championi Jumatatu, Jumatano, Ijumaa na Jumamosi ikiwa ni sehemu ya kukamilisha mafunzo yao.

Siku ya pili, wakiwa na shauku ya kujua mambo mengi, walikutana na mmoja wa wahariri waandamizi, Siafel Paul na kumuuliza mambo mbalimbali na kujibiwa sawia, jambo ambalo walishukuru kwa mapokezi na ushirikiano ambao wamepewa.

“Hakika tumejifunza mambo mengi, mengine ni tofauti kabisa na ambayo tulitaka kujua, tunashukuru kwa mapokezi na ushirikiano huu ambapo kwa kweli tumejifunza elimu kubwa mno,” walisema wanafunzi hao wakionesha moyo na siha za furaha.
(Habari: Brighton Masalu/GPL)