×

Banda kwaheri Simba, amalizana na Wasauz

IMEELEZWA kuwa, beki wa Simba, Abdi Banda, amejiunga na timu ya Baroka FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL) kwa mkataba wa miaka mitatu.

Kwa muda mrefu, Banda baada ya kumaliza mkataba ndani ya Simba, alikuwa kwenye mazungumzo na timu tatu za Afrika Kusini ambazo ni Chippa United, Bidvest Wits na Baroka. Rafiki wa karibu wa mchezaji huyo, ameliambia Championi Jumatano kuwa: “Banda tayari amemalizana na Baroka ambapo wale jamaa wametoa dola kadhaa kukamilisha usajili wake huo, inaonekana dau hilo lilikuwa zuri kwake ndiyo maana ameamua kusaini mkataba wa miaka mitatu.”

Championi Jumatano lilimtafuta meneja wa mchezaji huyo, Abdul Ahmed Boznia, ambapo alifunguka hivi: “Tayari kila kitu kimekamilika, Baroka walileta ofa nzuri ambayo ilionekana kuwazidi Bidvest.

“Unajua Bidvest walitaka kumpa mkataba wa mwaka mmoja, tukaona si sawa wakati tayari kuna timu imeleta ofa ya miaka mitatu, tukaamua kumalizana na Baroka ambapo akiwa huko, kila mwaka mshahara wake utakuwa unapanda.” Kwa sasa Banda yupo Afrika Kusini akiwa na Taifa Stars inayoshiriki michuano ya Baraza la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika (Cosafa) ambapo leo Jumatano watacheza dhidi ya Zambia katika hatua ya nusu fainali.

Leave a Comment