Kagera: Wajanja Wamemdanganya Mbaraka
UONGOZI wa Kagera Sugar umesema kuwa, kuna wajanja wachache wamejitokeza kumdanganya mshambuliaji wao Mbaraka Yusuph kwa lengo la kupiga fedha na kudai kuwa watakutana TFF na Azam kubaini nani mwenye haki.
Mbaraka ambaye amesaini Azam FC kwa mkataba wa miaka miwili, inasemekana ana mikataba ya aina mbili, ule wa miaka miwili na wa miaka mitatu Kagera Sugar, jambo ambalo linamuweka njia panda mchezaji huyo katika msimu ujao wa ligi kuu.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Meneja wa Kagera Sugar, Mohamed Hussein ameeleza kuwa kwa upande wao hawana neno, wanasubiria chombo chenye mamlaka TFF kiweze kutoa maamuzi juu ya mchezaji huyo ambaye ameingia chaka kutokana na wajanja wachache kumdanganya kwa ajili ya kupiga pesa.
“Jina la Mbaraka litajitokeza katika timu mbili msimu ujao lakini kwa upande wetu sisi hatuna la kusema, tunasubiria uchaguzi umalizike ili wahusika watoe maamuzi juu ya mchezaji huyo.
“Mchezaji ameshindwa kujitambua baada ya kuona amefanya vizuri na kusahau nyuma na kupata wajanja wachache waliomdanganya na kuamua kumpeleka Azam bila ya kuangalia mkataba wake wa huku, lakini mwisho wa siku TFF ndio watakaoamua.
“Kuna wakati Azam walikuja juu katika mtandao wao lakini wanapaswa kutambua kuwa kesi yetu sisi ipo na Mbaraka na si Kagera dhidi ya Azam kama wanavyoeleza kuwa wameona mkataba wake, hilo jambo halituhusu sisi, tunachojua ni mchezaji wetu halali.
“Sisi tulifanya mazungumzo na Simba na Yanga kwa ajili ya kumuuza huko lakini kabla hatujamalizana nao, kuna wajanja wamemchukua na kumpeleka Azam, ngoja tusubiri,” alisema Mohamed.
Championi lilifuatilia TFF kubaini ukweli juu ya jambo hilo, likataarifiwa kuwa mkataba wa Kagera na Mbaraka wa miaka miatatu ndiyo halali na siyo ule wa miaka miwili anaodai mchezaji.
Stori: Khadija Mngwai | Championi