
KATIKA miaka ya 2000, kulikuwa na ushindani mkali katika anga la Bongo Fleva, kwani kila siku kilizaliwa ‘kichwa’ ambacho kilikuja kuzidisha makali yaliyolifanya ‘game’ kuwa gumu.
Ukiacha ushindani mkubwa baina ya wasanii wenyewe, lakini pia kulikuwa na ligi nyingine baina ya watayarishaji wa muziki na waongozaji wa video za wasanii. Hata hivyo, wakati huo, watayarishaji na waongozaji walikuwa wachache tofauti na sasa.
Katika waongozaji wa video za wanamuziki, jina la John Kalaghe lilikuwa ni kubwa licha ya kwamba alikuwa ni kijana mdogo tu, akiwa amemaliza kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Azania, mwaka 2003 ambako pia alisoma kidato cha kwanza hadi cha nne.
Mshindani mkubwa wa John Kalaghe alikuwa ni Adam Juma wa Visual Lab na alitengeneza kazi za wasanii wengi baadhi yao wakiwa ni Dully Sykes (Kupenda) na Mrisho Mpoto ambaye video zake za nyimbo kama Salam kwa Mjomba, Nikipata Nauli, Adela na Narudi Kijijini.
Baada ya kuifanya kazi hiyo kwa miaka mitano, mwaka 2011 aliamua kuachana nayo na kujiingiza katika filamu, akiwa ameacha historia ya
kuwa Muongozaji Bora wa Video wa Mwaka 2008/09 kupata Tuzo za Kilimanjaro Music Awards.
Kupitia Kampuni ya Barazani Entertainments, Kalaghe kwa kushirikiana na wadau wengine, ameamua kujikita katika usambazaji ili kuwainua waigizaji, anaodai wameny-onywa kwa muda mrefu.
Risasi Mchanganyiko lilifanya mahojiano na mdau huyo wa muziki na ifuatayo ni sehemu ya mazungumzo yake.
Swali: Nini hasa sababu ya msingi ya wewe kuachana na utayarishaji wa video za muziki na kugeukia kwenye usambazaji wa filamu?
Kalaghe: Sababu ya msingi hasa ni kutokana na changamoto ya wasanii katika kulipana kazi. Nilichogundua wakati ule ni kwamba wasanii hawakuwa na uwezo wa kulipia video, kwa hiyo walikuwa wanategemea watu wengine.
Sasa unakuta mtu kaja na kazi yake, lakini malipo anafanya mtu mwingine, kwa mfano yule mtu kampa pesa yote lakini kwangu analeta kidogo, aliyetoa hela anapodai mbona video haioni, msanii anasema Kalaghe hataki kuiachia, kumbe sijamaliziwa pesa yangu.
Hili jambo lilinikosanisha na baadhi ya wasanii, halafu hata baadaye wadau kama Chief Kiumbe na Ustaadh Juma Namusoma walipojiondoa katika muziki, ndiyo kabisa, kama utakumbuka jamaa walikuwa wanawashika mikono wasanii wengi.
Swali: Lakini unakwenda kufanya kazi ya kusambaza filamu wakati soko lenyewe linakufa?
Kalaghe: Soko halijafa na haliwezi kufa. Hakuna siku utasikia muziki au filamu imekufa katika nchi yoyote, kinachotajwa kuwa kimekufa ni mawazo ya kuwafanya watu kutengeneza filamu zinazotazamika.
Watu wanataka sana filamu ila hawapati kile wanachokitaka. Mimi nimefanya utafiti na kugundua hiki ninachokuambia.
Swali: Watu kama Mtitu Game, 5 Effects, Kapico na wengine wamepumzika kuifanya hii kazi na wao ni wazoefu, wewe utawezaje?
Kalaghe: Kuhusu uzoefu, mimi nina uzoefu wa kutosha kabisa na isitoshe, mimi ni mmoja wa waanzilishi wa Steps Entertainment. Nimeshatengeneza filamu nyingi na najua pia naweza usambazaji na tumejipanga vizuri kabisa.
Swali: Unaweza kusambaza, lakini vipi kuhusu kazi bora, utatengeneza mwenyewe au itakuwaje.
Kalaghe: Barazani itakaa na wasanii na itawapa semina kuwaeleza kile ambacho tumekibaini katika tafiti mbalimbali. Tutaeleza ubora wa filamu maana yake nini na tutasambaza kazi za wale tu ambao watafikia vigezo vyetu.
Swali: Barazani imepata wapi uwezo wa kudiriki kuwasaidia kifedha wasanii katika kufanya kazi zao?
Kalaghe: Sisi tunapewa sapoti na taasisi ya TYEEO, ambayo inaundwa na Watanzania zaidi ya 200 na yenye miradi mingi. Tuliwapelekea wazo letu na wakatuelewa, kwa hiyo tutafanya nayo kazi.
Swali: Mmejaribu kujiuliza kwa nini wenzenu walishindwa kusambaza na nyinyi kupata njia mbadala?
Kalaghe: Sisi tunakuja na njia tofauti kabisa, tutafanya kazi kwa teknolojia, mtu ataweza kununua kazi kwa kutumia simu popote alipo atapelekewa mpaka barazani kwake. Kuna vijana zaidi ya 9000 watapata ajira kupitia mpango wetu wa usambazaji.
Swali: Wasanii wanalia kupunjwa au kudhulumiwa mapato kutokana na kazi zao kunakofanywa na wasambazaji, nyinyi mna tofauti gani.
Kalaghe: Uuzaji wetu utakuwa wa wazi kabisa. Msanii ataweza kuona kazi yake ilivyonunuliwa na hivyo atajua kiasi anachostahili. Kila mtu atafunguliwa akaunti yake kwenye mtandao na kupitia email yake ataona mauzo yanavyokwenda, sisi kama kampuni tutachukua asilimia yetu na wengine wote watachukua asilimia yao, wakiwemo waigizaji, madairekta, vijana wasambazaji mikoani, location manager na kila mtu atapata, lengo letu ni kila mmoja ajivunie na kuipenda kazi yake, hivyo kuwafanya wafanye vizuri zaidi.
Stori: Risasi Vibes| RISASI JUMATANO