
TIMU ya Mtibwa Sugar kutoka mkoani Morogoro imedai kuwa bahati tu ndiyo iliyowaokoa Ruvu Shooting chini ya Msemaji wao, Masau Bwire wasipate kichapo kutoka kwao kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara, Uwanja wa Mabatini, juzi Jumapili.
Timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 ambayo ilikuwa ni sare ya kwanza ya Mtibwa Sugar msimu huu, baada ya kutoka kushinda mechi tatu mfululizo za kwanza.
Katika mchezo huo, Ruvu ndiyo waliotangulia kupata bao dakika ya pili kupitia kwa Zuberi Dabi kabla ya Mtibwa kusawazisha kupitia kwa Stamili Mbonde dakika ya 55.

Akizungumza na Championi Jumatano, Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru, alisisitiza kuwa bahati ndiyo iliyowabeba Ruvu.
“Bahati tu ndiyo iliyowaokoa hawa Ruvu, umeona jinsi tulivyoutawala mchezo na umeona tulivyokuwa tukikosa mabao,” alisema Kifaru.