


NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula amewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri kuweka utaratibu wa kupanga miji kama sehemu ya kazi yao kuliko kukurupuka na mashinikizo ya makundi mbalimbali ya watu.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa madhimisho ya siku ya Makazi Duniani iliyofanyika katika Viwanja vya Karimjee Mabula alisema:
“Halmashauri ndio zinajukumu kubwa la kupanga miji lakini cha ajabu Halmashauri nyingi zimekuwa zikipima miji kwa mashinikizo ya makundi hali inayofanya kuibuka kwa miji holela mingi katika makazi yetu”
Ameongeza kuwa siku ya makazi inatukumbusha umuhimu wa kuwa na makazi bora yanayoendana na miundombinu ya huduma za kijamii.
Aidha ameeleza kwamba wizara yake imeweza kurasimisha nyumba zaidi ya 2000 katika eneo la Kimara na Mbezi lakini haijamaanisha kuwa zoezi hilo litaweza kuendelea nchi nzima katika maeneo ambayo yamejengwa kiholela.
Ameendeleea kueleza kwamba serikali itaendelea kusimamia mpango kabambe (Master Plan) wa miji yote hivyo hawatakuwa na msamaha kwa wote watakaokwenda kinyume na utaratibu wa mpango huo.