
WINGU zito limetanda na kuzua hofu kubwa moyoni mwangu. Natamani kuondoka mahali nilipo lakini naukosa mlango na kujikuta nikikaa kwa uchovu. Miguu haina nguvu huku tumbo la njaa likinisakama na kusema ukweli naanza kuishiwa na uvumilivu wa kuendelea kuwepo eneo hilo.
Wakati nawaza, ghafla mtu anachuchumaa mita chache sana kutoka mahali nilipokaa na anasogeza uso karibu na sikio langu.
Nainua kichwa na kumtazama usoni, oooh waoh. Ni Hussein Mkiety maarufu kwa jina la Sharo Milionea. Hapohapo sikujali tena ile hali ya uchovu na moja kwa moja mazungumzo yanachukua nafasi yake.
Sharo Milionea: Kijana hubadiliki!
Mimi: Kivipi tena kaka?
Sharo Milionea: Nilikuacha ukiwa mwembamba hivihivi na leo miaka mitano baadaye, uko vilevile au hauli, oooh mamaaa.
Mimi: (natabasamu) kila mtu na namna alivyoumbwa. Kwa upande wangu hata kama nitapata pesa nyingi kiasi gani kamwe siwezi kunenepa. Abadani!
Sharo Milionea: (anainuka na kujipangusa bega la upande wa kushoto na kisha anakaa tena), sijaachana na utozi wangu meeen, tena nikabaa… kabaaaaa…. Aiaiaiaiiii…mamamaa kapendekezwa…., kapendekezwa kuwa… wewe oooh mama… sawa, vipi huko kwenu kuna mtu amesharithi nafasi yangu ya U-milionea kwenye uchekeshaji?
Mimi: (nikiwa hoi kwa kicheko) kuna jamaa walijaribu kuja na staili yako lakini walishindwa, hakika pengo lako bado liko wazi kaka.
Sharo Milionea: Katika maisha huwezi kujifananisha na mtu yeyote, kila mtu aliumbwa kama alivyo na hata wewe hakuna mtu anayeweza kufanya mambo kama unayofanya wewe, yaani tumeumbwa kwa utofauti mkubwa sana lakini daaah! (anainama na kufunika uso kwa kiganja cha mkono wa kulia)
Mimi: Vipi tena kaka?
Sharo Milionea: Niliondoka huko kwenu nikiwa na shauku kubwa mno ya kufanya mapinduzi makubwa kwenye tasnia ya uchekeshaji, lakini safari yangu ya kuja huku ilikuwa ghafla na hadi leo huwa siamini kila nikipiga picha ya namna nilivyoondoka huko, halafu unajua ilikuwa tuwe pamoja na Kitale, lakini tulichengana kidogo tu, dah!
Mimi: Pole, wakati unaondoka duniani kuja huku, kulikuwa na bifu lililokuwa likitokota kati yako na Kitale, hebu fafanua kidogo ilikuwaje?
Sharo Milionea: Weee, acha habari zako za kidaku. Sijawahi na siwezi kuwa na bifu na Kitale hata kama akija huku leo. Siwezi kwa sababu ana mchango mkubwa mno kwenye mafanikio yangu. Ni yeye ndiye aliniibua na kunipeleka kwa Chuzi kabla hatujaanza kupiga kazi pamoja, kifupi ni mwalimu, rafiki na msaada wangu mkubwa, hatuwezi kuwa na bifu, You know what I’m saying…? Eeeh? Oooh Ma God… unasema nini jomba? Mmmh! Umebugi meeen.
Mimi: (tabasamu lililoambatana na kicheko kikavu). Ni filamu gani ambayo uliitendea haki na ilikuacha na kumbukumbu nzuri?
Sharo Milionea: (haraka sana) Power & Love ya Kanumba, kwanza ilikuwa mara ya kwanza kuigiza na msanii mkubwa kama yeye na hata aina ya stori yenyewe ilikuwa yenye kuumiza na kubwa zaidi ni kwamba mimi na yeye hatukudumu sana huko kwenu baada ya filamu kumalizika, mwenzangu alitangulia huku Aprili mimi Novemba nikamfuata, huwa tunatembeleana na kukumbushana mara kwa mara juu ya mambo mbalimbali huko duniani.
Mimi: Ni msanii gani wa vichekesho ambaye ulikuwa ukiigiza naye na kujisikia kweli ulikuwa kazini?
Sharo Milionea: King Majuto. Aise yule mzee ni kiboko! Nilikuwa nalazimika kutumia uwezo wangu wote kuhakikisha namfunika lakini weeee, anaku… anaku…. Anakubiiing na kukukunja namna hii (anainuka na kuanza kufanya manjonjo) yule mzee ni balaa. Vipi, kuna wachekeshaji wengine walioibuka baada ya mimi kuondoka ukiachana na akina Kitale, Bambo na wengine wazoefu wa zamani?
Mimi: Eeh, bwana. Siku hizi tuna akina Tin White wanatamba japo walikuwepo enzi zako lakini hawakuwa na umaarufu kama wakati wako, kuna Ebitoke, Katarina wa Karatu, Mau Fundi na wengine wengi wameibuka kaka.
Sharo Milionea: Hivi akina Joti, Masanja na wale wengine wapo?
Mimi: Wapo na Joti amefunga ndoa Jumamosi iliyopita, Masanja alishaoa kitambo na siku hizi yuko bize na kazi za Kichungaji na kuhusu hao wengine wapo. Nina kama miezi miwili tangu nionane na Alex Charamila au shemejiiiiii. Lakini hawafanyi tena shoo yao, kila mtu anapiga mishemishe zake.
Sharo Milionea: Mkwere na wenzake wapo? Mizengwe bado inaendelea? Vipi kuhusu rafiki yangu Musa Mateja bado yupo kazini maana yule jamaa damu zetu ziliendana sana.
Mimi: Mateja yupo na kuhusu Mkwere na wenzake wapo na kundi lao la Mizengwe linaendelea kama kawa kama dawa, kila Jumapili kitu kiko ‘laivu’ pale ITV.
Sharo Milionea: Safi sana. Naweza kukuagiza Tanga?
Mimi: Hapana kaka. Siku hizi nina kazi nyingi sana. Sitapata muda huo na ngoja nikutaarifu tu kwamba siku hizi niko pia upande wa Global TV Online na ofisi zetu tulishahama pale Bamaga- Mwenge, sasa hivi tuko Sinza- Mori, jengo la kisasa kabisa, picha hizi hapa (namtolea kamera na kumuonesha ofisi zetu mpya)
Sharo Milionea: Dah! Mmetisha sana. Kwa kweli Global mko serious na kazi. Ndugu yangu nilitamani sana tuendelee kuzungumza lakini muda hautoshi, nataka nikaonane na Mzee Small, aliniita mara moja nadhani anataka tuandae shoo ya uchekeshaji siku ya Uhuru, Desemba 9.
Mimi: Sawa bwana Sharo Milionea, lakini tunakukumbuka sana kaka. Dah! Hakika ulikuwa unachekesha na filamu yako ambayo sitaisahau ni ile ya Chumo uliyosimama na Yusuf Mlela na Jokate Mwegelo, dah! Bonge la filamu kaka na ulikuwa serious na siyo tena Sharo Milionea aliyekuwa amezoeleka, hongera kaka, msalimie sana Mzee Small, mwambie rafiki yake Saleh Ally anam-miss sana.
Sharo Millionea: Uwiii. Umenikumbusha Masalu. Ile filamu bwana nilionesha utofauti kabisa. Hivi Jokate yupo? Yusuf Mlela je? Ayaa nilikuwa nimewasahau kabisa wanangu wale, huku nako kunasahaulisha sana jamani. Wasalimie pia Chuzi na Kitale. Karibu basi na wewe huku. Karibu bwana kambi yetu ya milele hii.
Mimi: Acha mambo yako wewe. Muda wangu bado. Kwa heri bwana. Ghafla mlio wa simu yangu unapenya kwa kasi kwenye ngoma ya masikio yangu, nashtuka na kujikuta niko kitandani kwangu na hapohapo naitupilia mbali shuka na kukurupuka, kabla sijakimbilia bafuni kujiweka sawa tayari kwa safari ya kuelekea Sinza-Mori kuendeleza mbio za kufukuza ndoto kwa kufanya kazi.
Usishtuke sana, simulizi hii si halisi bali ni ndoto tu na nimekufikirisha kiburudani zaidi.
Kwa maoni na ushauri nicheki kwa namba hizi; 0673 42 38 45.