
NI wazi kwamba tuko kwenye kipindi ambacho maisha yanataka akili ifanye kazi zaidi ya kawaida (extraordinary thinking). Mambo yamekuwa magumu kwa kila namna kiasi cha watu wengi kuchanganyikiwa na hii si kwa Tanzania pekee, bali sehemu nyingi duniani, kuna ugumu wa uchumi. Hapa tunakuletea mbinu na kanuni za kutumia ili kuvuka kipindi hiki ambacho watu wamekibatiza jina la ‘vyuma vimekaza’.
1: WAZO BORA LA BIASHARA
Watu wengi wakisikia neno biashara, jambo la kwanza ambalo huwaijia kichwani ni mtaji. Nilichobaini neno mtaji limekuwa ‘ukuta’ na kikwazo kikubwa cha watu kutimiza ndoto zao na kufikia vilele vya mafanikio. Kitu cha muhimu katika kujinasua na wakati mgumu kiuchumi ni kuwa na wazo bora la biashara. Ufafanuzi yakinifu; maana halisi ya biashara haiishii kwenye kununua na kuuza bidhaa. Biashara ni kitendo cha kutoa huduma yenye kuhitajika sana kwa jamii. Maana yake hata kama huna mtaji wa pesa, ukajitolea kuamka asubuhi kisha ukaenda kufanya usafi wa kukata majani na kuondoa takataka kwenye majumba ya watu, ni lazima watakulipa. Ninachomaanisha hapa ni kuangalia tatizo ambalo limekuwa ni kero kwa jamii unayoishi na kutafuta namna ya kuliondoa.
Katika ugumu wowote wa uchumi, wakati ambapo wengi wanakiri na kulalamika pesa kukata mifukoni mwao, wewe umiza zaidi akili kutoa huduma ambayo hata kama mtu ana pesa kidogo ni lazima apate huduma yako. Ngoja nifafanue kwa mfano halisi. Pengine mtaani kwako kumejaa maduka yanayouza maji ya kunywa, kuanzia shilingi 600 na kuendelea, lakini ukitazama wakazi wengi wa eneo hilo uwezo wao wa kununua maji kwa bei hiyo zaidi ya mara moja ni mgumu na wewe unajua kabisa kuna maji ya bomba ambayo hayana chumvi mahali fulani, kwa nini usiyachukue maji hayo na kuyaweka kwenye vyombo maalum kama chupa safi na kuyaweka kwenye friji ambapo unakuwa unauza kwa shilingi 200? Huoni kama utakuwa unatengeneza nafasi ya kujipatia pesa? Ninasisitiza uumize akili kupata wazo bora la biashara ambayo iko kwenye kundi la mahitaji ya lazima ya kila siku ya watu.
Kabla sijamalizana na kipengele hiki, ninataka nikupe mfano mmoja mfupi wa msichana ambaye alilazimika kuachana na masomo ya shule ya msingi kwa sababu ya wazazi wake kukosa uwezo wa kumsomesha na wakati huo bibi yake alikuwa mgonjwa wa kansa hivyo pesa kidogo iliyopatikana kwa familia iliishia kwenye chakula na matibabu ya mgonjwa.
Ni katika kipindi ambacho yuko nyumbani, binti huyo akawa anamhudumia bibi yake kwa mahitaji yote. Kadiri siku zilivyosonga ndivyo alijikuta akipenda sana kuhudumia wagonjwa na hapohapo akapata wazo la kutoa huduma kwa wagonjwa wakiwa nyumbani. Akaandika tangazo na kulibandika mtaani kwao, kwamba kama kuna familia yenye mgonjwa asiyejiweza yeye
yuko tayari kumhudumia.
Kuanzia hapo akawa anapata oda zaidi ya ishirini kwa siku na hatimaye kuanzisha kampuni ya kutoa huduma kwa wagojwa majumbani, leo hii ni miongoni mwa wanawake wanaotajwa kuwa na pesa nyingi katika nchi ya Marekani. Wakati vyuma vimekaza, wewe amsha akili yako kutatua mahitaji muhimu, lazima pesa zikufuate hata kama huzitaki! Mtaji wa kupata pesa zaidi uko nyuma ya kichwa chako, hapo kisogoni. Ndiyo, ninamaanisha akili yako ina majibu ya kila kitu unachokihitaji maishani. Ingia kazini na jitolee kikamilifu, pesa inapenda sana jasho halali la mtu. Mtu mmoja aliwahi kubanwa na haja kubwa akiwa stendi ya basi. Alihangaika sana kutatua tatizo hilo, hadi aliposaidiwa na watu waliokuwa wakiishi karibu na eneo la stendi, kuanzia hapo alianzisha wazo la kujenga vyoo stendi ya mabasi, leo hii kuna pesa inapatikana kupitia huduma ya vyoo na kuoga kwenye stendi za mabasi, tumia akili yako kukukwamua na mkazo wa vyuma.
2: ONGEZA UBUNIFU
Hakuna biashara mpya! Nyingi zilishafanywa, lakini hiyo isikupe shida. Muhimu ni wewe kuongeza ubunifu kwenye biashara yako. Ijumaa ya wiki iliyopita, nilikwenda kula gengeni, lakini niliondoka na elimu kubwa sana kuhusu ubunifu. Mwanzoni nilikaa peke yangu, lakini ndani ya muda mfupi sana viti vyote vilijaa wateja, lakini wauzaji wa pembeni hawakuwa na watu kabisa. Nikaanza kufanya utafiti unaomfanya yule mama auze kuliko wenzake ndipo nikabaini jambo moja. Yule mama anaweka maji ya kunywa kwenye kidumu cha lita tano, kwa hiyo mteja akimaliza kula hatoi pesa mfukoni kununua maji ya kunywa, lakini wauzaji wengine hawakuwa na maji, mteja akimaliza kula inamlazimu kwenda kununua maji wakati bei ya chakula ni sawa na ya mama mwenye maji kwenye dumu, nani ataacha kwenda kula kwenye maji ya kunywa ambayo halipii?
Kwa hiyo hakikisha unakuwa mbunifu sana kwenye biashara yako. Hata kama umeajiriwa, hiki ni kipindi ambacho waajiri wengi wanajitahidi sana kubaki na wafanyakazi ambao wanazalisha zaidi kuliko wategeaji na wanaofanya kazi kwa mazoea na ndiyo maana makampuni mengi yamepunguza wafanyakazi, si kwa lengo baya, lakini ni kutaka kubaki na wenye tija, ambao hata kama wanalipwa pesa nyingi, lakini wanaizalishia kampuni. Kuwa mtu wa kipekee kwenye eneo lako la kazi na biashara. Kama unauza maembe kwa mfano, hakikisha unakuwa mbunifu kuanzia kwenye kifaa au mahali pa kuuzia.
Usafi wa mazingira na wewe unakuwa wa kiwango kikubwa. Weka maji safi ya kunawa kwa ajili ya wateja wanaokula hapohapo, menya kwa ustadi mkubwa na kwa wanaonunua na kuondoka, wafungie kwenye mfuko safi na onesha unyenyekevu na ukarimu wa hali ya juu, ni lazima watu wajazane kwako na hapo utakuwa unajitengenezea pesa licha ya watu wengine kubaki wakilalamikia ugumu wa maisha huku wakibaki vijiweni wakijadili siasa za nani kahamia chama gani, wewe unapiga pesa tu.
Ndugu zangu, maisha ni mchakamchaka. Hakuna kusimama, ni kama mwendesha baiskeli ambaye ataacha kunyonga pedeli na baiskeli itasimama na hatimaye ataanguka. Pambana na maisha kwa kuwa mbunifu kwa kila ulifanyalo ili uendelee kupata pesa kwenye kipindi chochote kigumu, kamwe usifanye mambo kwa mazoea, zama na nyakati hizo zilishapita zamani mno. Narudia tena, umiza akili kwa kiwango kisichotamkwa.
Katika kipindi kama hiki, unapataje usingizi? Tunatofautiana sana. Yaani kama kuna mtu anavuta shuka na kukoroma kabisa hadi asubuhi, basi anayafaidi sana maisha! Wengine hatukumbuki mara ya mwisho kulala usingizi wa pono ilikuwa lini! Kuwa wa kipekee kwenye kila eneo. Kama umepewa kazi ya kufagia, fagia hadi malaika wa zamu waseme kwa sauti kwamba hapa alifagia mtu! Kama una biashara ya kufua nguo majumbani kwa watu, fua hadi nguo zenyewe zijisikie kweli zimefuliwa. Kifupi ni kwamba, kuwa mbunifu kupitiliza na pesa zitajaa mfukoni mwako kupitiliza!
3: JIWEKEE NEMBO BORA
Wazungu huita jambo hili kwa jina la brand. Kwenye bidhaa au kazi zako jiwekee nembo ya kudumu ambayo itakuwa utambulisho wako. Ifike mahali kama mtu anahitaji huduma yako, ajue moja kwa moja wewe umejikita kwenye eneo gani. Mfano, Rais wa Marekani wa sasa na mfanyabiashara mkubwa, Donald Trump anajua faida ya nembo. Jina lake linatumiwa na wafanyabiashara wengi mno duniani na wanamlipa pesa nyingi. Kuna wanaotengeneza tai na kuziandika jina lake, wengine wanatengeneza mvinyo (wine) na kuziita kwa jina lake na bidhaa zingine nyingi. Na wewe ninakushauri ujiwekee nembo bora ya kudumu katika kazi zako. Mfano hapa nchini, ukitaja neno hadithi, asilimia tisini ya Watanzania watakutajia Shigongo, ingawa kuna wengine wa vizazi vya nyuma kama marehemu Ben Mtobwa na Elvis Musiba. Watu hawa walijitengenezea nembo kwenye eneo hilo, maisha ni kujitambua wewe ni nani na umekuja kufanya nini duniani, pambana kutimiza malengo ya wewe kuzaliwa.
4: TENGENEZA MTANDAO
Jitahidi sana kujitanua kwa kufahamiana na watu wengi kadiri uwezavyo. Mipango au kama ambavyo vijana wa kisasa huita michongo mingi iko kwa watu. Kadiri unavyofahamiana na watu wengi ndivyo unavyojiongezea fursa nyingi za kujipatia pesa kwa sababu wingi wa kufahamika kwako na biashara yako ni wingi na ongezeko la wateja na pesa!
5: NIDHAMU
Nidhamu imegawanyika katika makundi makuu matatu. Nidhamu kwa watu, muda na pesa. Mfanyabiashara yeyote kama hana nidhamu ni vigumu mno kupiga hatua zaidi. Ni lazima ujiwekee nidhamu kwa watu. Heshimu watu wote ingawa usipitilize na kuwa kama unawaabudu. Mchukulie kila aliye mbele yako kama sababu ya wewe kufungua biashara yako. Ona kabisa kutoka moyoni mwako kwamba bila yeye usingeanzisha biashara kwa sababu umefungua biashara hiyo ili uhudumie watu, sasa kama watu hao huwaheshimu, unadhani wao watakuheshimu wewe na kujali biashara yako? Jibu unalo.
6: ONDOA KABISA MATUMIZI YASIYOKUWA YA LAZIMA
Hiki ni kipengele ambacho huwashinda watu wengi sana. Hivi karibuni nilipata nafasi ya kumsikiliza tajiri wa Kitanzania kijana zaidi, Mohamed Dewji ‘Mo’ juu ya namna ambavyo hutumia pesa zake. Hakika nilibaki mdomo wazi na nikajifunza kabisa kwamba kumbe matajiri hawana matumizi ya kufuja kama ilivyo kwa masikini ambao utapanyaji wao wa pesa ni mkubwa tofauti kabisa na vipato vyao. Mo anasema: “Ninanunua vitu vya muhimu sana ambavyo ni lazima viniache na faida maishani mwangu, ninaishi kawaida mno na kuielekeza akili kwenye kuongeza pesa nyingi zaidi kuliko kuitumia zaidi kwa matumizi yasiyokuwa na tija.” Itaendelea wiki ijayo. Imeandaliwa na Brighton Masalu, 0673 42 38 45.