










Chuo cha Sayansi ya Afya cha Kahama, mkoani Shinyanga, leo kimefanya mahafali yake ya kwanza kwa kishindo ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Fadhili Nkulu, pia katika hafla hiyo chuo kilimwalika mgeni maalum, Dkt. Louis Shika, kutoka jijini Dar es Salaam ambaye aliwasili leo kwa ndege.
Dkt. Shika ambaye amekuwa maarufu nchini kama ‘bilionea wa nyumba za Lugumi’, alipokelewa kwa shangwe na kuzungushwa katika msafara mrefu katika mji wa Kahama na watu waliokuwa wamepanda bodaboda na magari ambapo alipofika chuoni hapo alishangiliwa na wanafunzi.
Wahitimu na walimu chuoni walimpongeza Dkt. Shika kwa umaarufu aliojipatia katika mnada huo ambapo sasa ameibua neno maarufu la ‘900 Itapendeza’.
Ifuatayo chini ni risala ya chuo iliyosomwa kwa mgeni rasmi katika mahafali hayo:
RISALA YA MAHAFALI YA KWANZA KWA WAHITIMU WA UFAMASIA HATUA YA MSINGI ( BASIC TECHNICIAN CERTFICATE IN PHARMACEUTICAL SCIENCES NTA LEVEL 4 2017)
Mheshimiwa mgeni rasmi, viongozi mbalimbali wa serikali,Mkurugenzi wa chuo,watumishi wa chuo,wageni waalikwa,wazazi,wahitimu,wanachuo, mabibi na mabwana,Tumsifu Yesu Kristo,Bwana Yesu Asifiwe, Assalam Alaykum.
Mheshimiwa mgeni rasmi, awali ya yote tunayo furaha na heshima kubwa kwa kuitikia mwaliko wetu katika mahafali yetu ya kwanza katika Chuo hiki cha Sayansi za Afya kahama. Karibu sana, jisikie uko nyumbani.
Mheshimiwa mgeni rasmi, hii ni mahafali yetu ya kwanza tangu chuo hiki kilipoanzishwa mwaka 2016. Huu ulikuwa ni uamzi wa hekima na busara kwa Mkurugenzi wetu wa chuo Ndugu Yona Bakungile, wadau kutoka sehemu mbalimbali hapa Kahama, pamoja na Wizara ya Afya.Tunashukuru sana tena sana kwa dhati kabisa kwa uamzi huo mzuri.
Mheshimiwa mgeni rasmi, Chuo Cha Sayansi za Afya Kahama (Kahama College of Health Sciences) ni chuo cha binafsi kinachotoa mafunzo ya Utabibu na ufamasia kwa ngazi ya Astashahada na Stashahada chini ya miongozo na sera za Wizara ya Afya Tanzania. Chuo hiki kilianza kutoa mafunzo baada ya kupata usajili wa kudumu wenye namba REG/HAS/171 mwaka 2016. Tulianza na jumla ya wanafunzi 157 kwa kozi zote kwa mwaka wa masomo 2016/2017 na hadi sasa tuna jumla ya wanafunzi 257 kwa mwaka huu wa masomo 2017/2018
Mheshimiwa mgeni rasmi, mbele yako ni wanafunzi wapatao 30 wanaohitimu masomo yao leo katika kozi ya Mafunzo ya Msingi ya ufamasia (Basic Technician Certificate in Pharmaceutical Sciences). Hakika vijana hawa wamepata mafunzo bora ambayo yatawawezesha kuingia kwenye soko la ajira ndani na nje ya nchi. Na baadhi yao tayari wameshapata ajira sehemu mbalimbali hapa nchini na wanafanya kazi zao vizuri. Tunawapongeza sana pia kulingana na mtaala wao wa Wizara vijana hawa wataendelea na ngazi ya cheti na Diploma hadi chuo kikuu kwa watakaomudu.
Mheshimiwa mgeni rasmi, Chuo cha Sayansi za Afya Kahama kina mazingira mazuri na rafiki kwa kujifunzia kwani kina miundombinu bora na ya kisasa kama kinavyoonekana. Hivyo chuo hiki kinalenga zaidi katika kutoa wahitimu bora na watakaokuwa na uwezo mkubwa wa kutatua changamoto zinazoikabili jamii na taifa kwa ujumla.Hata hivyo chuo hiki kina mahusiano mazuri sana na Hospitali ya Mji wa Kahama na taasisi zingine za afya kwani wanafunzi wetu hupokelewa vizuri wanapofanya mafunzo kwa vitendo. Sisi wafanyakazi wa chuo tunawaahidi wazazi, walezi na wanafunzi kuwa tutawapa kilicho bora, watahitimu wakiwa wameiva na mahiri. Tunachowaomba tu ni ushirikiano wa dhati kutoka kwao. Maana tunaamini tabia njema na mafanikio huenda sambamba.
Mheshimiwa mgeni rasmi, katika uendeshaji wa chuo tunakutana na changamoto mbalimbali zikiwemo:
- Kupokea idadi ndogo ya wanafunzi ukilinganisha na wale tuliowadahili kwa sababu ya wazazi na walezi kukosa mwamko wa elimu.
- Kupata wanafunzi wenye nia na dhamira ya kweli ya kusoma lakini hawana uwezo wa kulipa ada na gharama zingine kwa sababu wanatoka familia masikini sana na wengine ni yatima au kuwa na mzazi mmoja asiye na uwezo wa kumudu gharama kabisa.
- Wanafunzi wanaoendelea na masomo kushindwa kulipa gharama na hivyo kufanya uendeshaji wa chuo kuwa mgumu.
- Upatikanaji wa vitabu nchini ikiwa ni pamoja na vifaa vya mafunzo kwa vitendo (Skill lab) kitu ambacho kinatulazimu kuagiza nchi za nje. Pamoja na hayo Chuo kinajitahidi kutumia vitabu vilivyopo, ikiwemo njia mbadala ya computer kwa kupitia nakala laini.
OMBI: Mheshimiwa mgeni rasmi, tunaomba utusaidie kupata wahisani na wadau mbalimbali ambao wanaweza kusaidia watoto wanaotoka familia masikini na zisizo na uwezo wa kumudu gharama ili nao waweze kupenya na kupata hii elimu bora. Ambayo itasaidia nchi yetu kuwa na watalaamu wengi katika idara ya afya na kusaidia watanzania kuwa na afya njema ili kuendana na sera ya Tanzania ya viwanda.
Mheshimiwa mgeni rasmi,
Tukushukuru wewe binafsi kwa kuacha kazi zako nyingi na kuja kujumuika nasi katika shughuli hii muhimu ya kuwaaga vijana wetu. Tukuombe tena pindi upatapo mwaliko usisite kuja kujumuika nasi.
Ahsante sana!
MKUU WA CHUO,
CHUO CHA SAYANSI ZA AFYA KAHAMA
PICHA NA HILALY DAUDI/GPL-GLOBAL TV ONLINE