×

Nyerere Ashtuka Kusikia ‘Vyuma Vimekaza’

NGURUMO na pepo kali zinaongezeka. Sauti za migongano ya miamba zinaendelea kuyapa shida masikio yangu, huku baridi nayo ikisumbuana na ngozi yangu laini. Wakati napambana na hali hiyo, ghafla nashikwa mkono kwa nguvu na hapohapo naketishwa chini bila kumtazama usoni anayefanya hivyo.

Dakika mbili baadaye, nalazimika kumuangalia mtu huyo. Akili inahamaki baada ya kujua anayeniongoza ni mtu ninayemjua, Samuel Sitta.

 

Sitta: Hujambo? Mwalimu Nyerere anakuita, nifuate. (nainuka bila kusema chochote na kumfuata kwa nyuma hadi kwenye eneo tulivu lenye kila kitu, sofa ambazo sina maneno ya kuzieleza na meza iliyotengenezwa kwa madini nisiyoyajua, mbele ameketi Mwalimu Nyerere na hapohapo anaanza kuniuliza maswali). Mwalimu Nyerere: Unaonekana mgeni eneo hili, unaitwa nani?

 

Mimi: Naitwa Masalu, mwandishi wa habari kutoka Global Publishers, nafikiri unaifahamu vizuri.

 

Mwalimu Nyerere: Naikumbuka vizuri niliishuhudia ikiwa ndio inazaliwa! Enhe, Sitta aliniambia baada ya Kikwete kumaliza muda wake wa urais kuna mtu anaitwa Dk. Magufuli ndiye rais wa nchi yetu, maisha yakoje huko chini ya uongozi wake?

Mimi: Mambo yanakwenda safi kabisa. Aliingia na mabadiliko ambayo yalilenga kutupeleka pazuri. Kwa sasa anaendelea kupambana kuhakikisha nchi yetu inakuwa yenye neema na kila Mtanzania anaifaidi keki ya taifa, hakika anaonesha uzalendo ambao nasikia ulikuwa nao wewe, maana wakati wa utawala wako sikuwepo.

 

Mwalimu Nyerere: Sana yule kijana sikuwahi kufanya naye kazi kwa karibu lakini niliona ana ndoto kama yangu, niliambiwa hata na Sitta hapa lakini ili kujiridhisha ikabidi nikuulize na wewe na pia nilielezwa makali yake na kina Deo Filikunjombe, George Kahama, Joseph Mungai na wengine wengi tu wanaomfahamu vizuri.

 

Mimi: Rais Magufuli amedhamiria kuibadilisha Tanzania ambayo uliitamani kwa miaka mingi, kifupi ni kwamba anafanya yale ambayo kuna wakati ulitamani yafanyike ukiwa hai.

 

Mwalimu Nyerere: Kama yapi hayo kijana? Wewe si umesema wakati wa utawala wangu hukuwepo, sasa ni
mambo gani ambayo unasema nilitamani yafanyike nikiwa hai lakini haikuwezekana na Magufuli ameyafanikisha?

 

Mimi: Yapo mengi lakini nitakutajia machache kwa leo.

 

Mwalimu: (akijiweka sawa kwenye sofa na kuishika vyema fimbo yake huku akinikazia macho), nakusikiliza mwanangu.

 

Mimi: Ulitamani sana serikali yote ihamie Mjini Dodoma, yalipo makao makuu. Yaani wizara zote na watumishi wake waishi huko, haikuwezekana kwako lakini hadi sasa hakuna waziri anayeishi Dar na hata Waziri Mkuu wa sasa anaishi Dodoma na kila kitu kiko huko.

 

Mwalimu Nyerere: (ananyanyuka na kutoka mara moja, anarejea akiwa ameshika picha ya Rais Dk. Magufuli), huyu kijana amefanya hayo? Mbona Sitta hukuniambia haya (anamtupia macho Samuel Sitta, kisha anayarudisha kwangu), hadi waziri mkuu amehamia Dodoma? Basi serikali yote iko Dodoma kwa sababu waziri mkuu ndiye mtendaji mkuu wa serikali, safi sana aiseee, (kicheko kile cha kutingisha mabega, anakuna pua na kuketi tena)

 

Mimi: Hivi mwalimu uliwezaje kung’atuka madarakani kwa hiyari yako, wakati ule hakukuwa na mfumo wa vyama vingi na hukujilimbikizia mali nyingi kama ilivyo kwa viongozi wengi wa Bara la Afrika wanaong’ang’ania madaraka huku wakivuna ukwasi wa kutisha?

Mwalimu Nyerere: (anacheka tena na kununa ghafla), sikutaka kujilimbikizia mali kwa sababu sina roho ya ufisadi na uchoyo, nilipigania haki na uhuru wetu kwa ajili ya vizazi vya baadaye kama ninyi sasa hivi.

 

Ningeweza kujimilikisha madhahabu yote na kila kilicho cha thamani, lakini sikufanya hivyo hata kidogo, unaweza kukumbuka hata ile nyumba ya Butiama, sikutaka lakini Jeshi la Kujenga Taifa likasema mwalimu bwanaaa, unajuaaa, lelelelele, nikasema basi lakini kusema, kusema, kusema ule ukweli sikua na hiyari hiyo (anaendelea)… Kuhusu madaraka, kwa nini ning’ang’anie madaraka hata nishindwe kufanya mambo kwa ufanisi nikatenda yale ya kijinga? Hata siwezi mimi na kama kuna kiongozi wa namna hiyo basi ujue iko shida, tena si kidogo kabisa.

 

Samuel wewe unaweza kuwa shahidi kwa namna ambavyo nilikuwa nasisitiza viongozi kupokezana vijiti (anaendelea na swali) Mwalimu Nyerere: Maendeleo gani mengine anayafanya Dk. Magufuli?

 

Mimi: Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wenye jina lako yaani Mwalimu Julius Nyerere, kwa sasa umepanuliwa na una terminal tatu ingawa hiyo ya tatu haijakamilika, pale Ubungo kuna ujenzi wa barabara za juu (Interchange) na pale Tazara kuna ujenzi wa aina hiyo, ile Barabara ya Ali Hassan Mwinyi ilishapanuliwa mno, wanafunzi kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne wanasoma bure (naendelea huku nikihema) Watumishi wa serikali wameongeza nidhamu ya kazi, hakuna wafanyakazi hewa tena, wale wazungu waliozoea kutunyonya kwa madini yetu, wametia adabu, pale Kigamboni kuna daraja la kuvuka kwa miguu na magari kutoka Posta kwenda Kigamboni. Tuna ndege zetu mpya; Bombadier, na nyingine zimeshaagizwa zipo njiani.

 

Mwalimu Nyerere: Aiseee, kumbe, sasa nchi yetu imepata kiongozi bora, nakiona kitu cha tofauti kwake!

 

Mimi: Si hivyo tu, siku hizi tuna mabasi yaendayo kasi. Kuna pia ujenzi wa reli ya umeme (standard gauge), bandari inafanya mambo kwa ufanisi kabisa, hakuna tena wiziwizi, kifupi mwalimu nchi yetu iko kwenye mabadiliko makubwa kuelekea kwenye neema ya asali na maziwa, ngoja tumpe muda zaidi. Sasa hivi watu wote ni kazi tu. Vyuma vimekaza kwa vijana wasiokuwa watafutaji.

 

Mwalimu Nyerere: Vyuma ndio nini we kijana? Mimi: Hahahaha! Huo ni msemo wa kisasa, unamaanisha hali ni ngumu hususan kwa wale ambao walikuwa wakiishi kiujanjaujanja.

 

Mwalimu Nyerere: Daah! Vijana mna mambo sana. Enhe, Ben (Mkapa) yupo? Samuel (Malecela) naye je? Salim Ahmed Salim yuko wapi? Mwinyi hazeeki? Mama Maria anaendeleaje? Mwanangu Makongoro anafanya nini sasa hivi? Warioba mzima? Halafu Kingunge hajambo? Nilisikia Edward (Lowassa) alihamia Chadema wanaendeleaje huko? Yule kiongozi wao Edwin (Mtei) naye yupo?

 

Mimi: (najikuna kichwani kidogo kisha namjibu kwa kujiamini) wote wapo mwalimu. Mwanao Makongoro aliomba ridhaa ya kugombea urais lakini kura hazikutosha, Lowassa ndo hivyo yupo Chadema kwa sasa na Kingunge yupo lakini siku hizi yuko kimya sana. Mtei yupo. Salim Ahmed Salim yupo, naye yupo kimya pia. (hapohapo najikuta nikikurupuka, naamka na kuachana na kitanda, kumbe mazungumzo yangu na Mwalimu Nyerere ilikuwa ni ndoto)

Kwa maoni na ushauri nicheki kwa namba hizi; 0673 42 38 45.

NA BRIGHTON MASALU | GLOBAL PUBLISHERS | SAA TISA USIKU KITANDANI KWANGU

Leave a Comment