×

Spoti Xtra Lazidi Kushika Kasi Kitaa

GAZETI jipya la michezo la Spoti Xtra ambalo ni gazeti dada la Championi, jana Jumapili lilizidi kucha­nja mbuga mitaani na kugombewa na waso­maji baada ya kutoka kwa mara ya pili am­bapo mara ya kwanza lilitoka Jumapili iliyopita ambapo halikuchukua raundi na kumalizwa mapema na wasomaji wa habari za michezo.

Kama ilivyokuwa wiki iliyopita, jana pia kulikuwa na msafara wa kuzunguka mitaani kuzidi kulitangaza gazeti hilo lililojizolea umaarufu mkubwa ndani ya muda mfupi kutokana na habari zake za michezo na burudani za ndani na nje ya nchi, uchambuzi wa michezo kutoka kwa wachambuzi mahiri, hadithi za kusisimua kutoka kwa watunzi mahiri, picha zenye ubora na mengineyo mengi ya kuvutia.

Msafara huo ulianzia ofisi za gazeti hili zilizopo Sinza Mori na kuelekea maeneo ya Mwenge, Kinondoni, Kigogo, Ilala Boma, Karume, Keko, Tandika, Temeke Mwisho na kuhitimisha msafara huo Kiwanja cha Taifa cha Burudani cha Dar Live baada rudo la magazeti hayo yaliyokuwa yakiuzwa kumalizwa na wasomaji.

Baadhi ya wasomaji waliokuwa kwenye magari zikiwemo daladala walionekana kuwaomba madereva kusimamisha magari hayo ili kwanza wajipatie Spoti Xtra ndiyo safari iendelee.

Richard Bukos, Dar es Salaam.