×

Banza Stone Aanika Uadui, Urafiki Wake na Chocky!

Banza Stone enzi za uhai wake.

KILA nikifumba macho nawaona kwa mbali malaika wananiita. Akili inajenga picha niko kwenye jeneza tayari kwenda kuzikwa, hapohapo nakurupuka lakini nakumbana na mazingira ya ajabu mno. Vumbi la ajabu! Kelele kila mahali na vishindo visivyoeleweka vinasikika kwa fujo.

Naamua kukaa na kusikilizia nini kinaendelea. Kikohozi cha kuondoa hewa nzito mdomoni kinatawala na hapohapo naguswa bega na mikono ya baridi ambayo naipapasa na kugundua ni myembamba mno.

Banza Stone: Wewe mdaku na huku unafanya nini?

Mimi: Aaaah, mzee wa kitimtim vipi kwema?

Banza Stone: Salama, niaje huko utokako?

Mimi: Salama kabisa kaka, lakini kuondoka kwako kulituumiza sana kwa kweli.

Banza Stone: Kawaida na hayo ndiyo maisha, vipi Chocky yupo?

Mimi: Amejaa tele kaka. Umemkumbuka sana?

Banza Stone: Mimi na Chocky tena! Tuna historia ndefu sana kaka.

Mimi: Kivipi?

Ally Chocky.

Banza Stone: Kwanza, tulianza kufanya kazi pamoja kwenye Bantu Group lakini mimi nilikuwa maarufu kumshinda yeye, baadaye tukahamia Twanga Pepeta ambako nilizidi kumfunika na alikuwa chini yangu kwa kila kitu (anakohoa kidogo na kuweka mkono mdomono akiwa amekunja ngumi kuzuia kikohozi chake kisiwe kero kwangu), lakini nilinunuliwa kwa dau kubwa sana na TOT.

Mimi: Wakati huo nilikuwa kijijini nakimbizana na ngedere sijui chochote kuhusu muziki (anacheka na kunigusa kwa mkono huku akinitazama usoni).

Banza Stone: Wewe ni kijana mzuri sana, unasema ukweli maana kuna watu huwa wanajifanya wanajua mambo kumbe hawajuji chochote na mbaya zaidi hawajui kama hawajui.

Mimi: Hebu nieleze kidogo upinzani wako na Chocky ulikuwaje?

Banza Stone: Nilipoondoka Twanga na kumuacha Chocky, alipandishwa na kuwa kiongozi na mimi nikapewa uongozi kule TOT, ushindani ukawa wa nguvu kwa kiwango kisichotamkwa.

Mimi: (huku nikijiweka sawa kwa kujifuta michanga kwa viganja vya mkono wa kushoto), ikawaje?

Banza Stone: Tuliingia kwenye upinzani mkubwa sana hadi ikafikia kipindi tukawa tunaitana majina ya ajabu sana. Mimi nilikuwa namuita Cho** na yeye akawa ananiita teja! Nakumbuka siku moja tulishindanishwa pale kwenye Ukumbi wa Vijana, niliposhika maiki nikasema kwa nguvu Choo** halafu mashabiki wakamalizia na neno… (tusi) yaani na yeye alipopanda jukwaani alianza na neno teeeee halafu mashabiki wakamalizia kwa maneno ya jaaaaa yaani teja!

Mimi: Aisee mlifika mbali sana kaka, baadaye ikawaje?

Banza Stone: Upinzani uliendelea kwenye nyimbo, wakati huo nikaachia madude yenye kishindo kikali kama Elimu ya Mjinga, Simba na nyingine nyingi tu, lakini haikuishia hapo likaandaliwa shindano jingine tena pale Diamond Jubilee na Chocky aliingia na tingatinga na ndiyo maana kwenye wimbo wa Elimu ya Mjinga nimesema kwenye starehe kijiko kimefikaje? Tingatinga limefikaje? Yaani mimi na Chocky ilikuwa kama Ray na Kanumba kwenye filamu zao au Simba na Yanga.

Mimi: Mwisho ilikuwaje sasa kaka?

Banza Stone: Niliondoka TOT na kuanzisha bendi yangu nikaiita Bambino Sound, wewe acha tu ndugu yangu lakini haikudumu nikajiunga na Twanga ambapo Chocky aliondoka na kuhamia kwingine.

Mimi: Aisee wewe na Chocky mlikuwa na ushindani mkubwa sana.

Banza Stone: Chocky alikuwa adui lakini pia alikuwa rafiki wa ajabu sana kwangu.

Mimi: Kivipi?

Banza Stone: Ninaposema alikuwa adui maana yake ni kwamba kwenye kazi tulikuwa na uadui wa kushindana lakini kwenye maisha halisi alikuwa mshikaji na kwenye matatizo alijitoa sana na ndiyo maana ninamuita adui na rafiki wa ajabu na kama una kumbukumbu nzuri siku za mwisho wa uhai wangu nilikuwa nafanya kazi chini yake akiwa bosi wangu kwenye Bendi ya Extra Bongo.

Mimi: Kweli kabisa, nakumbuka kaka.

Banza Stone: Vipi, ndugu zangu wapo?

Mimi: Ndiyo, huwa napita pale Sinza-Lion na kuwaona ndugu zako hususan yule kaka yako na mama wakiwa nje maana pale ni barabarani sana.

Banza Stone: Kweli, ukienda wasalimie sana. Msalimie pia Asha Baraka na umwambie namshukuru sana kwa kila alichonifanyia maishani mwangu kabla sijaja huku. Yule ni mwanamke wa chuma kwelikweli, Mungu atamlipa kwa wakati.

Mimi: Asante lakini kuna kitu nataka nikuulize kaka… (maneno hayo nayatamka nikiwa nimekaa kitandani na ninafumbua macho na kujikuta niko kitandani kwangu, kumbe ilikuwa ndoto iliyonikutanisha na gwiji la Muzuki wa Dansi, Banza Stone. Sina jinsi zaidi ya kuweka mambo sawa na kuwahi kazini kupambana na maisha.)

Maoni na ushauri: 0673 42 38 45.

Makala: Brighton Masalu | SAA 9 USIKU KITANDANI MWANGU!