NÉLSON de Jesus Silva ndiyo jina lake halisi, lakini watu wa mpira walimfahamu zaidi kwa jina la Dida. Enzi zake akicheza soka, Dida, raia wa Brazil, alijulikana kama muokoa penalti hatari sana.
Dida anakumbukwa zaidi kwa kile alichoifanyia AC Milan alipoichezea kwa miaka kumi kuanzia 2000 hadi 2010. Huko ndiko aliponyanyua jina lake na hatimaye akafahamika kama mmoja wa makipa bora zaidi duniani. Alikuwa na uwezo mkubwa sana wa kuzuia mashuti, na kutawala eneo lake la kudaka.
Dida alishinda mataji mengi ya klabu pamoja na binafsi akiwa na AC Milan, lakini pamoja na ubora wake huo, alijulikana pia kwa kufanya makosa mengi.
Katika kikosi cha Milan, ndipo aliposhinda taji la Ligi Kuu ya Italia (Serie A) na Ligi ya Mabingwa Ulaya mara mbili, huku ubingwa wake wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa ukitokana na kuokoa penalti tatu katika fainali ya mwaka 2003 dhidi ya mahasimu wao wa Italia, Juventus ambapo Milan ilishinda kwa penalti 3-2.
Kwenye ngazi ya kimataifa, Dida aliichezea Brazil mechi 91 katika kipindi cha miaka 11 kuanzia 1995 hadi 2006, akishinda Kombe la Dunia na medali ya Olimpiki.
Lakini kumbuka kuwa huyu ni mchezaji mwenye mafanikio makubwa zaidi katika historia ya Kombe la Mabara. Dida alistaafu timu ya taifa baada ya Brazil kuondolewa katika Kombe la Dunia 2006 katika hatua ya robo fainali.
Akitajwa kama mmoja wa makipa bora wa kizazi chake, Dida ni kipa wa kwanza wa Kibrazili kutajwa katika Tuzo za Mchezaji Bora wa Dunia (Ballon d’Or), huyu ni mchezaji wa kwanza kushinda Kombe la Dunia la Klabu mara mbili, na alitajwa mara saba katika tuzo za kipa bora zinazoandaliwa na Shirikisho la Kimataifa la Historia ya Soka na Takwimu (IFFHS), na ni mmoja wa wachezaji tisa tu waliowahi kushinda Ligi ya Mabingwa na Copa Libertadores.
Huyu ni kipa wa sita kwa ubora katika karne ya 21 kwa mujibu wa takwimu za IFFHS. Na anatajwa kama mmoja wa makipa bora waliowahi kuidakia Brazil akiwa na Marcos, Rogério Ceni, Cláudio Taffarel na Gilmar.
Dida aliipaisha sana hadhi ya makipa weusi katika soka la Brazil kutokana na mafanikio aliyoyapata Ulaya, kwani awali walikuwa wakibaguliwa na kutengwa.
Gwiji huyu alistaafu soka mwaka 2015 akiwa na kikosi cha Internacional cha nchini Brazil, akiwa na umri wa miaka 42.
MATAJI
Cruzeiro:
Copa Oro: 1995
Copa do Brasil: 1996
Copa Libertadores: 1997
CORINTHIANS:
Campeonato Brasileiro: 1999
Kombe la Dunia la Klabu: 2000
Torneio Rio-São Paulo: 2002
Copa do Brasil: 2002
MILAN:
Serie A: 2003–04
Coppa Italia: 2002–03
Supercoppa Italiana: 2004
Ligi ya Mabingwa Ulaya: 2002–03, 2006–07
Uefa Super Cup: 2003, 2007
Kombe la Dunia la Klabu: 2007
BRAZIL:
Michuano ya Vijana Amerika Kusini: 1992
Kombe la Dunia la Vijana: 1993
Copa América: 1999
Kombe la Dunia: 2002
Kombe la Mabara: 1997, 2005
TUZO BINAFSI:
Medali ya Fedha ya Kipa Bora wa Dunia wa IFFHS: 2005
Medali ya Shaba ya Kipa Bora wa Dunia wa IFFHS: 2004
Kipa Bora wa Mwaka Serie A: 2003–04
MAISHA BINAFSI
Dida amekuwa msiri sana na mambo yake binafsi, lakini inasemekana ana mke mmoja (Lucia) na mtoto mmoja. Desemba 18, 2013, Dida alipata uraia wa nchi nyingine, Italia, hivyo ana uraia wan chi mbili.
ANACHOKIFANYA KWA SASA
Dida amekuwa akifanya shughuli mbalimbali za kuinua vipaji vya watoto. Pia ana taasisi kadhaa za kusaidia jamii na michezo, mwaka 2014 yeye pamoja na Juan na Andrés D’Alessandro walianzisha taasisi ya Pan American Health Organization, ambayo inalenga kupunguza magonjwa.
Mwaka 2013, akiwa pamoja na mastaa wenzake wa zamani wa Brazil,
Rogério Ceni, Gilberto Silva, pamoja na wachezaji wenzake wa zamani wa Milan, Clarence Seedorf na Alexandre Pato, walianzisha Common Sense FC, taasisi yenye lengo la kuwatetea wachezaji katika soka la Brazil wawe wanapata fidia zao kwa wakati.
KLABU ALIZOCHEZEA
MWAKA KLABU MECHI MABAO
1992–1993 Vitória 24 0
1994–1998 Cruzeiro 188 0
1998–1999 Lugano 0 0
1999–2000 Corinthians 40 0
2000–2010 Milan 302 0
2001–2002 Corinthians (mkopo) 35 0
2012 Portuguesa 32 0
2013 Grêmio 60 0
2014–2015 Internacional 41 0
Jumla 722 0