×

Kengele ya Hatari Imewaka kwa Simba SC, Yanga

BAADA ya makelele mengi na tambo za huku na kule katika dirisha la usajili lililofungwa Agosti 31, mwaka huu hatimaye wadau wa soka wamefanikiwa kuwaona ‘Majayanti’ ya soka la Tanzania klabu za Simba na Yanga kwa msimu ujao.

 

Walianza Yanga siku ya Agosti 29, mwaka huu pale kwenye Uwanja wa Mkapa ambapo katika kilele cha wiki ya Mwananchi mbele ya klabu ya Zanaco kutokea nchini Zambia walikumbana na kipigo cha mabao 2-1.

 

Watu wakasema hiko ni kipimo kizuri kuelekea michezo yao miwili ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United ya Nigeria. Bahati mbaya kwa Yanga na Tanzania kwa ujumla Yanga wakapoteza michezo yao yote miwili kwa kufungwa bao 1-0 kila mchezo na kutolewa kwenye michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu Afrika.

 

Kwa upande wa Simba nao Jumapili iliyopita ya Septemba 19, walikuwa na jambo lao pale kwa Mkapa katika kilele cha siku ya Simba ‘Simba Day’ ambapo waliwaalika mabingwa mara tano wa Ligi ya Mabingwa Afrika klabu ya TP Mazembe ya DR Congo.

 

Simba walikuwa na siku nzuri sana hasa unapozungumzia mafanikio ya Tamasha lao hilo, ambalo lilifanyika kwa mara ya 13 mfululizo, lakini kwa bahati mbaya kwao mwishoni mchezo huo ukaisha kwa Simba kufungwa bao 1-0.

 

Kimsingi matamasha yamekwisha na matokeo ndo kama tulivyoyashuhudia, kilichopo mbele yetu kwa sasa ni msimu mpya wa 2021/22 ambao unatarajiwa kuanza kutimua vumbi kuanzia Septemba 27, mwaka huu.

 

Katika kuonyesha kuwa mambo yanazidi kupamba moto wababe hao wawili Jumamosi hii watakuwa na mchezo wa Ngao ya Jamii utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam ambao kikanuni ndiyo kufunguliwa rasmi kwa msimu mpya wa ligi.

 

Baada ya matamasha haya kupita, dhana ya umoja ni ya muhimu zaidi kuliko kutengana kwani hakuna muda wa kulaumiana zaidi ya yote kila timu ifanye tathimini ya yale mazuri yao, ili kuyaendeleza katika michezo ijayo huku wakijitahidi kurekebisha changamoto zilizojitokeza ili zisijirudie katika michezo ijayo.

 

Tayari tumeanza kuona viashiria vya baadhi ya mashabiki wa klabu hizi wakiwa na kampeni za chinichini, za kulaumu baadhi ya watendaji wa klabu zao kama vile viongozi, mabenchi ya ufundi na hata baadhi kuwataja wachezaji.

 

Presha hii imeonekana kuwa kubwa zaidi hasa kwa upande wa Yanga, na kupelekea kuwepo kwa baadhi ya hatua kama mabadiliko kadhaa katika benchi la ufundi, hali ambayo inaweza kuwa na athari kubwa kwa malengo yao ya muda mfupi na malengo ya muda mrefu.

 

Kiufundi Yanga walikuwa na wakati mgumu sana kuandaa timu yao, uongozi umejitahidi sana kusajili nyota wa viwango vya juu karibu katika kila nafasi uwanjani na hata kocha mkuu, Nasreddine Nabi aliandaa programu nzuri ya kikosi chake lakini tatizo kubwa likawa kwenye muda wa maandalizi.

 

Tumeongea sana kuhusu safari ya Yanga nchini Morocco, na sioni kama bado kuna ulazima wa kulizungumzia hilo lakini ukweli ni kwamba katika hili Yanga walifanya makosa makubwa.

 

Yanga ya sasa inahitaji muunganiko wa pamoja wa kitimu ili kuweza kutoa matokeo chanya uwanjani, na ili kulifanikisha hilo ni jambo la muhimu sana kwa Wanayanga kuisapoti timu yao kuliko kulaumu.

 

Lakini hata kipigo walichopata Simba kutoka kwa TP Mazembe kina mengi ya kuyaeleza hususani maoni ya kocha mkuu, Didier Gomes juu ya safu yake ya ushambuliaji ambayo ni wazi ilikosa umakini wa kutumia nafasi walizotengeneza, lakini Simba pia walionekana kukosa ule muunganiko wao wa msimu uliopita bila shaka hii ni kutokana na ingizo la nyota wapya.

 

TP Mazembe waliwapa Simba mechi nzuri ya kupima ubavu wao hasa katika michuano ya kimataifa, msimu uliopita Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika walifika hatua ya robo fainali, na kwa msimu huu wana malengo ya kufika angalau nusu fainali ya michuano hiyo mikubwa Afrika.

 

Ni wazi vipigo ambavyo Simba na Yanga wamevipata katika michezo yao iliyopita, vinapaswa kuchukuliwa kama kengele ya tahadhari kwao kwa msimu ujao ili wasije kurudia makosa hayo na hatimaye kufanya vizuri.

Leave a Comment