
MUNGU wa mbinguni amefumbata fungu lako la mafanikio kiganjani mwake. Wakati wako ukifika, kila kitu kitakaa sawa na unachotakiwa kufanya ni kuchapa kazi kwa nguvu na kutimiza yote yaliyo ndani ya uwezo wako na kuyakabidhi mikononi mwa Mungu yaliyo juu ya utashi wa kibinadamu! Maisha ni mapambano na ni vita kali kushinda ile ya mabomu ya nyuklia. Pambana vizuri na tumia kila mbinu uijuayo, lakini iwe halali!
Leo nahitimisha somo hili la nidhamu. Nilianza kufundisha nidhamu ya muda, nikafundisha nidhamu ya fedha na hapa ninamalizia na nidhamu ya watu. Nasisitiza tena, hakuna unachoweza kufanya katika ulimwengu wa mafanikio bila kuwa na nidhamu. Hili ndilo daraja pekee la kuvuka kwenda kwenye hatma ya mafanikio yako.
Msomaji, mafanikio makubwa unayoyaota yako mikononi mwa watu. Unaota kuwa mfanyabiashara mkubwa, kwani biashara hiyo utaifanya na akina nani kama siyo watu? Unataka kuwauzia akina nani bidhaa zako? Jibu ni jepesi kabisa kwamba chochote unachotaka kukifanya ni kwa ajili ya watu. Kwa hiyo unapaswa kuwa na nidhamu ya watu kwa kiwango chote.
Waheshimu watu wote bila kujali rangi, dini, kabila wala umri. Kamwe usiwe mtu wa kubagua watu wa kuwaheshimu kwa sababu za kimazingira. Eti unamheshimu mtu fulani kwa sababu ya maslahi binafsi. Kwa ufafanuzi ni kwamba, kuna baadhi ya watu huheshimu watu kwa sababu anajua mwisho wa siku kuna faida ataipata kupitia mtu huyo, huo ni unafiki uliopitiliza.
Unajinyenyekeza kwa mtu kwa sababu ana pesa au kwa sababu ni bosi katika kitengo chako cha kazi, kwa sababu unajua kwa kufanya hivyo kuna faida utazipata kupitia mtu huyo. Huko ni kujipendekeza na hakuna dhambi mbaya katika maisha ya utafutaji wa mafanikio kama kujipendekeza kwa mtu! Heshimu yeyote apitaye mbele yako. Hujui ni nani atakuwa na msaada gani kwa mazingira yapi na lini utamhitaji katika maisha yako.
Maisha tunayoishi ni ya kutegemeana. Hata kama umejaliwa kuwa na mali nyingi kiasi gani, unadhani hizo pesa zitakufaa nini kama huna heshima na nidhamu kwa watu? Unadhani ukionesha nidhamu kwa mtu utapungukiwa nini? Lazima uhakikishe unakuwa na nidhamu kwa watu wote uwajuao na usiowajua.
Katika kitabu chake cha The Art of Deal, Rais Donald Trump wa Marekani anasema: “Discipline is the only bridge to success, in my organization if you any situation of indiscipline, then you are fired.” (Nidhamu ndiyo daraja pekee la kuelekea kwenye mafanikio, kwenye kampuni yangu kama wewe ni mfanyakazi na ukaonesha viashiria vyovyote vya utovu wa nidhamu, basi huna kazi.)
Huo ndiyo msingi na msisitizo wa nidhamu katika maisha. Shuka chini kadiri uwezavyo na utakula matunda ya nidhamu yako. Matajiri na watu wote unawajua duniani walioifanikiwa, sijui akina Oprah Winfrey, Shakira, Jay Z, Ronaldo, Kobe Brayant, LeBron James, Carlos Slim, Mack Zuckerburg na wengineo wengi, ni kwamba wamefika hapo kwa sababu walitanguliza nidhamu mbele, nidhamu kwa watu wote na leo hii wanaogelea kwenye dimbwi kubwa la utajiri, wakifurahia maisha.
Kama wewe ni mfanyabiasahara, ni muhimu kuweka nidhamu kwa watu ili upate ramani na ‘michongo’ ya kusaka maisha kupitia watu. Kama huna nidhamu, yaani wewe ni mtu wa nyodo, majigambo na dharau ni nani atakukaribia na kukupa mawazo mapya ya biashara? Kwa hiyo, faida kubwa ya nidhamu nikufungua milango ya watu kukusogelea na kukupa mawazo ambayo ukiyafanyia kazi, unajikuta umeingia kwenye ramani nzuri ya mafanikio.
LAKINI NIDHAMU ISIPITE KIWANGO!
Nalazimika kutoa ufafanuzi zaidi ili kuondoa mkanganyiko. Isitokee mtu akaamua sasa kutumia neno nidhamu kwa mazingira ambayo hayafai. Labda niseme tu, licha ya kuwa nimesisitiza umuhimu wa mtu kuwa na nidhamu hususan kwenye maisha ya kupigania mafanikio, lakini niwe tu mkweli kwamba kuna watu hawastahili kabisa kupewa nidhamu! Ndiyo, wakati mwingine ni vizuri katika maisha kupeana maneno makali, lakini yemejaa ukweli na uhalisia katika maisha.
Watu ni wa ajabu. Ukiwaonesha upole na nidhamu kwa unyenyekevu wote, wanatumia nafasi hiyo kukudharau na kukukandamiza kwa namna ambayo wao wanaona inafaa. Kuna tofauti kubwa kati ya heshima na nidhamu. Heshima ni ukomo wa mazoea juu ya jambo au mtu fulani kutokana na nafasi au umri na hekima ni kujizuia na kujinyima kufanya jambo kwa ajili ya kulinda hadhi ya utu. Vyote ni muhimu katika maisha, lakini kubwa sana ni afadhali kuwa na nidhamu kuliko kuwa na heshima, ambayo mwisho wa siku ina ukomo wa muda. Hili nalo ni somo kubwa tu ambalo nitalifundisha siku zijazo.
Watu wanaumiza ndugu zangu. Wapo ambao huamua kutumia nafasi zao kikazi au kiumri kuwaumiza kwa kuwaonea wenzao kwa sababu wanaamini hawana cha kuwafanya. Mtu kama huyo hata kama anakuzidi umri au cheo kazini, lakini hastahili kabisa nidhamu, zaidi sana waheshimu tu pindi wanapokuwa machoni pako.
Lakini pia kuna wengine hawastahili hata hiyo heshima, zaidi sana wanafaa kuoneshwa hofu tu ili maisha yasonge. Huko mbele nitakuwa na vitu vingi sana vya kufundisha. Kwa hiyo usiruhusu watu watumie mwanya wa nidhamu yako kukuumiza. Kama wewe ni mfanyabiashara, eti mtu anakuja kuchukua bidhaa bila utaratibu na wewe unakaa kimya kwa kuwa eti unaonesha nidhamu kwake, ukifanya hivyo utashangaza ulimwengu.
Kuwa na nidhamu kwa kiwango kinachohitajika, lakini upole na nidhamu hiyo visigeuke fimbo ya watu kukupiga. Hakikisha unakuwa imara. Penye kuonesha nidhamu, fanya hivyo, lakini panapostahili kuiweka nidhamu pembeni, fanya hivyo na onesha makucha yako yote, ilimradi tu uko sahihi kwa unachokipigania.
Ndugu zangu, ulimwengu wa kutafuta fedha unahitaji watu wenye roho ngumu. Watu wasiokuwa wapole sana. Unapaswa kuwa mtu mwenye moyo wa ujasiri na ‘roho mbaya’ kwa baadhi ya mambo ili uimudu fedha. Mafanikio hayataki watu lelemama, watu lainilaini na wenye huruma kupindukia. Ndiyo maana watu wengi walio wapole na wasiopenda makuu, mafanikio kwao huwa ni magumu (simaanishi waliofanikiwa wote wana roho mbaya na siyo wapole), ninachomaanisha hapa ni kwamba, maisha ya utafutaji yanamtaka mtu apunguze sana huruma na awe na ngozi ngumu na moyo wa kupigania haki yake bila kujali anamuudhi nani, ilimradi tu asivunje sheria za nchi wala kumdhalilisha mtu kwa namna yoyote.
SASA TUHITIMISHE HIVI
Unataka kuwa nani katika maisha haya? Sema basi! Nini kinakuzuia? Hakuna ni wewe tu. Unakwama wapi? Sikiliza, mchawi wa maisha yako ni wewe mwenyewe. Hakuna mtu wa kumlaumu. Dunia imejaa fedha nyingi ambazo zinakusubiri wewe tu unyanyuke na upige hatua kuzikamata.
Huna mtaji? Hicho ni kisingizio cha kizamani! Mbona unaniabisha namna hii wewe? Mtaji mbona unao, tena mkubwa tu! Unataka nikuoneshe mahali ambapo mtaji wako upo? Usijali, mimi na wewe tena! Hebu nyanyua mkono wako wa kulia na ukishike kichwa chako. Safi sana, shika upande wa nyuma kidogo, ehee, teremesha mkono chini kidogo, hapohapo. Ndani ya hicho kisogo chako ndipo umejificha mtaji wako wa mamilioni unaouhitaji. Hapo ndipo penye hazina yako.
Maana yangu ni kwamba, akili uliyonayo ndiyo zawadi pekee ambayo Mungu alikupa ili ikuongoze kuamua ni aina gani ya maisha unataka kuishi. Akili zetu ni mtaji mkubwa mno. Muhimu ni wewe kutumia akili yako kuwaza ni jambo gani unaweza kulifanya na likakuingizia fedha? Nimeshafundisha suala hili huko nyuma kwa hiyo sitaki kurudia.
Kwanza, chukia umaskini. Lazima uwe na sababu ya wewe kufanikiwa. Sababu namba moja iwe ni kuchukizwa na umaskini na kuanzia hapo, utakuwa na hasira kali sana ya kusaka fedha ili uondokane na maisha hayo ya kubangaiza. Kama kuna watu wanakudharau na kukucheka kwa sababu ya umaskini wako, hao ndiyo kuni za kuchochea moto wako wa kuyatafuta mafanikio na ukishayakamata ndiyo kaa la moto vifuani mwa waliokuwa wanakucheka huko nyuma.
Hatua ya pili ni kuamua unataka nini maishani. Ukishajua unachokitaka tayari ni hatua ya kwanza kuelekea kwenye mafanikio. Jiwekee malengo na mikakati ya namna ya kukipata hicho unachokitaka. Kinachofuata hapo ni wewe kuingia kwenye mchakato wa kutenda kwa kutumia mbinu na mikakati hiyo.
Baada ya hapo, jiandae kukutana na changamoto, lakini usivunjike moyo na hatimaye utajikuta ukifika mahali unapotaka kufika. Kuwa na nidhamu na matumizi ya muda wako, kamwe usikubali kupoteza muda kwa kufanya mambo yasiyokuwa na tija na ambayo hayakusaidii kuleta mafanikio.
Matumizi bora ya fedha na nidhamu kwa watu. Kumbuka kuwasaidia wasiojiweza, saidia mlemavu yule, tembelea wagonjwa majumbani na hospitalini. Msaidie mjane yule hata kwa kumlipia mwanaye ada au kumnunulia mwanaye viatu vya shule. Kuwa malaika kwa watu wengine, Mungu amekupa fedha hizo siyo za kwako tu, amempa mtu kupitia mikono yako, usizibanie, zitakukimbia!
Sifael Paul. Huyu ni mhariri wa gazeti hili, lakini ni miongoni mwa watu wanaoingia kweye orodha ya marafiki zangu kutokana na fikra zajke chanya kuhusu maisha na mafanikio. Wiki iliyopita, nilipata nafasi ya kuzungumza naye kwa kirefu sana kuhusu vijana na maisha. Tukawa tunajadili namna ambavyo nchi yetu ya Tanzania imejaa fursa nyingi mno za mtu yeyote aliyedhamiria kufanikiwa.
Sifael akawa ananieleza vitu ambavyo nilihamasika sana kushiriki na ninyi wasomaji wangu ili sote kwa pamoja tuzidi kulisukuma gurudumu la mafanikio. Wiki ijayo nitaanza kutoa somo maalum kabisa kuhusu fursa zilizopo nchini mwetu na namna ambavyo tunaweza kuzitumia katika kujiletea maendeleo. Usikose.
Kwa mawasiliano na ushauri, tuwasiliane kwa namba hizi; 0679 65 96 33.