
NIMEENDELEA kufuatilia mechi mbalimbali za Ligi Kuu Bara inayoendelea kutimua vumbi kwenye viwanja mbalimbali nchini.
Naona upinzani unazidi kuongezeka na hata ukiangalia msimamo wa ligi hiyo, utaona kwamba timu hazijaachana kwa pointi nyingi kuanzia zile zilizopo kileleni zinazowania ubingwa na zile zilizo upande wa pili zinazowania kutoshuka daraja.
Kwa jinsi ilivyo hadi sasa, huwezi kutabiri ni timu gani itashuka daraja, wala huwezi kutabiri ni timu gani itatwaa ubingwa.
Yanga imekuwa gumzo kwa wiki za hivi karibuni kutokana na kuonekana imepotea njia katika ramani ya ubingwa.
Yanga ina pointi 25 katika nafasi ya tatu, ilitoka sare dhidi ya Mwadui kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kuwashangaza wengi kwa sababu kabla ya hapo ilifahamika kwamba Mwadui ni vibonde wa Yanga; wacheze Shinyanga au Dar es Salaam.

Hata ushindi ambao Yanga iliupata wikiendi iliyopita dhidi ya Ruvu Shooting wengi waliuona kama wa kubahatisha, kwa sababu Ruvu Shooting walikosa nafasi nyingi zaidi lakini Yanga ndiyo iliyofanikiwa kushinda kwa bao moja lililofungwa na Pius Buswita.
Nikiitazama Yanga niseme wazi kuwa timu haina morali. Unapoitazama Yanga ikicheza hauoni upambanaji, hauoni kujituma, hauoni watu wakitafuta ushindi.
Yanga wanacheza kama watoto yatima, kama watu waliotelekezwa. Inawezekana wana matatizo mengi nje ya uwanja, hasa ya kiuchumi, bila shaka ni kutokana na mwenyekiti Yusuf Manji kuwa nje ya timu kwa sasa.
Kila mara huwa nawasisitiza wachezaji na ningependa kuwasisitiza tena kuwa hautakiwi kuyaingiza matatizo ndani ya uwanja.
Unapoingia uwanjani, kila mara hakikisha akili yako inakuwa sawa, hakikisha upo sawa kisaikolojia na kimwili, kwa sababu hiyo ndiyo kazi yako na hapo uwanjani ndipo unapotengenezea fedha na jina na heshima na fursa.
Simba hivi sasa wanaonekana wapo katika morali ya juu, na inaonekana itakuwa vigumu sana kuwashusha kwa sababu wana kila kitu.
Yanga wanatakiwa watambue kuwa kama timu ikiwa inashinda mashabiki huongezeka, lakini ikifanya vibaya wanapungua.
Najua kwamba kutetea ubingwa ni kazi kubwa, tena kama ukiwa unapitia changamoto kama ambazo Yanga inazipitia hivi sasa.
Ukiangalia msimamo, Simba imeiacha Yanga kwa tofauti ya pointi saba, wengi wameanza kudai kwamba tayari Yanga imeshaondoka kwenye mbio za ubingwa, lakini wanasahau kwamba mpira hauko hivyo.
Msimu uliopita, katika mzunguko wa kwanza, kabla ya mechi mbili za mwisho Simba ilikuwa inaongoza kwa tofauti ya pointi nane dhidi ya Yanga lakini ikapoteza mechi mbili mfululizo na ikabaki tofauti ya pointi mbili, mwisho wa siku Yanga ikatwaa ubingwa.
Ndiyo maana nasema hadi sasa huwezi kujua ni timu gani itatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.
Bado hata raundi ya kwanza haijaisha, kwa hiyo tusubiri tuone kitakachotokea, lakini hadi sasa naweza kusema kwamba Simba wapo vizuri zaidi kimorali kuliko Yanga.
Simba na Yanga zinatarajiwa kushiriki michuano ya kimataifa mwezi ujao, ukiangalia mambo yanavyotokea kwenye ligi utaona ni kitu gani ambacho timu hizo zitakwenda kukifanya katika michuano hiyo.
Unajua mpira unachezwa hadharani, na kila mtu anaona, hivyo tayari picha tumeshaipata juu ya kile ambacho timu hizo zitakwenda kukifanya katika michuano ya kimataifa.
Naamini Simba na Yanga zitafanya vizuri katika michuano ya kimataifa.
Yanga nina wasiwasi nayo kidogo, inatakiwa viongozi, wachezaji na mashabiki washikamane, na viongozi wajitahidi kutatua kero za wachezaji wao ili waingie uwanjani na kutumika kwa morali.
Wakicheza michuano ya kimataifa kama wanavyocheza hivi sasa, basi kuna uwezekano mkubwa wa kufeli.
Bado kuna muda wa kujiandaa na kurekebisha dosari ndogondogo katika vikosi hivyo ili viweze kuliwakilisha vyema taifa letu.
Nimalizie kwa kuipongeza timu ya JKT Ruvu au JKT Tanzania kama inavyofahamika siku hizi kwa kuwa timu ya kwanza kupanda daraja kutoka Ligi Daraja la Kwanza kwenda Ligi Kuu Bara msimu ujao.
Kila mtu anajua ushindani uliopo katika Ligi Daraja la Kwanza, kwa hiyo JKT kufanikiwa kupanda ni matokeo ya maandalizi mazuri na nidhamu ya wachezaji na viongozi ndani na nje ya uwanja.
Halafu kurejea kwa kocha Bakari Shime katika kikosi hicho baada ya muda mrefu kuwa bize na Serengeti Boys, kuliwapa nguvu JKT, hivyo wakafanya kazi yao kwa umakini mkubwa na kufanikiwa walichokilenga.
Wito wangu kwa vyombo husika, TFF au Bodi ya Ligi ni kuwa katika kutafuta hizi timu tano zilizobaki kwa ajili ya kupanda daraja, basi ufuatiliaji uwe mkubwa ili kusiwepo na aina yoyote ya kubebana wala kupindisha haki na kufanya fitina ili baadhi ya timu zipande kwa kubebwa.
Stori Mohammed Hussein , Mawasiliano +255 789 343 414