BENCHI la ufundi la Yanga chini ya kocha wake mkuu, George Lwandamina raia wa Zambia limeeleza kutofurahia ratiba ya kikosi chake kinachokabiliwa na mchezo mgumu wa marudiano Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers ugenini nchini Botswana.
Yanga leo Jumatatu itashuka uwanjani kucheza na Stand United ya Shinyanga ikiwa ni siku mbili tu Ijumaa iliyopita kucheza na Kagera Sugar kwenye mchezo wa ligi huku Yanga wakishinda kwa mabao 3-0.
Kikosi hicho pia Jumamosi hii kitakuwa na kibarua cha kucheza ugenini dhidi ya Township Rollers ya Botswana katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo Yanga kwenye mchezo wa kwanza walipoteza kwa mabao 2-1.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Mzambia huyo amesema anahofia kutopata muda wa kutosha kuwaandaa wachezaji wake kwa ajili ya mchezo huo ambao ni lazima Yanga iibuke na ushindi wa mabao matatu ugenini ili iweze kufuzu hatua ya makundi.
Said All, Dar es Salaam