×

Riadha Tanzania Hii Ni Aibu Kubwa

WAKATI wanari­adha kutoka dun­iani wamekusanyika hapa Valencia, Hispania tayari kwa Mashindano Makubwa ya Dunia ya Riadha Nusu Mara­thon, Tanzania imekosa mwak­ilishi.

 

Tanzania kabla ilikuwa iwakil­ishwe na Wanariadha tisa, kabla baadaye kukutana na ‘zengwe’ la wanariadha hao ambao ni watumishi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kuitwa kam­bini kwa ajili ya kwenda kwenye mafunzo ya kijeshi na baadaye kubaki wawili ambao wangewak­ilisha, nao wamegonga mwamba.

 

Taarifa za kugonga mwamba kwa hao wawili ambao ni Ezekiel Ngimba na Jacklin Sakilu ambao nao wote wanatoka katika timu ya Jeshi la Wananchi (JWTZ), zimetolewa hapa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) Wilhelm Gidabuday, am­baye amesema wanariadha hao wamekosa ruhusa kazini kwao.

 

Hili ni pigo kubwa kwa mchezo huu ambao miaka ya nyuma ul­ituletea heshima kubwa kabisa, lakini sasa unaelekea kabisa kupotea na kuwaachia wenzetu wa Kenya watambe wanavyowe­za na mchezo huu.

 

Gidabuday amelazimika kuja hapa Valencia akiwa mikono mitu­pu bila ya wanariadha na amekuja kuhudhuria mkutano tu huku nchi kadhaa duniani wakiwemo majira­ni zetu Kenya, Uganda, Ethiopia na Rwanda, wanariadha wake wapo hapa tayari kwa mashindano haya ya dunia ya Nusu Marathon.

 

Kuna mtu mmoja aliwahi kuse­ma aliyeturoga katika michezo amekufa, inawezekana niliichuku­lia kauli hii kuwa ni utani lakini sasa naiona kama ina ukweli. Hivi kweli wanariadha wananyimwa ruhusa ya kuja hapa? Hapa wa­likuwa wanakuja kulipigania taifa na kama tungepata medali sifa ingeenda kwa taifa lakini leo hii tunabaki wasindikizaji.

 

Mashindano haya yangetumika pia kwa maandalizi kwa vijana wetu kabla ya kwenda Gold Coast, Australia mwezi ujao katika mich­ezo ya Jumuiya ya Madola. Kweli bado tuna ndoto ya kuja kupata medali hapo mbele? Hakika tuna safari ndefu sana.

Wakati wenzetu wanatumia michezo kama kichocheo cha ajira siye tunaiona haina thamani kabisa, sijui lini tutaamka katika usingizi mzito tuliolala.

 

Kama tunashindwa kuleta timu katika mashindano makubwa kama haya hata wenzetu wanat­uonaje?

Wanaikumbuka ile Tanzania ya zamani iliyokuwa na wanariadha wakaleta heshima duniani. Tanzania ya akina Filbert Bayi, Selemani Mu­jaya Nyambui na akina Gidamis Sha­hanga leo iko wapi?

Hawa walipambana na kuleta heshima na kujenga majina ambayo mpaka leo kwenye medani ya Riad­ha yanakumbukwa.

 

Kama tumeshindwa kuleta wa­nariadha hapa na wakapambane na kujiandaa vyema kwa michezo ya Jumuiya ya Madola mwezi ujao na Olimpiki mwaka 2020 Tokyo, Japan kuna haja ya kwenda pia huko? Hilo ndio swali nimekaa nawaza wakati mbele yangu nikiwaona wanariadha wa Kenya wakiwa wamewasili hapa na tambo kibao za kuchukua medali.

 

Ndoto za mwanariadha Alfonce Felix Simbu ambaye alikuwa anata­ka kutuletea medali nyingine kupitia mashindano haya na yale ya Japan ya Olimpiki zimeyayuka.

 

Simbu ni miongoni mwa wa­nariadha waliokuwa wanajianda na mbio hizi za Valencia kabla ya kuitwa kambini jeshini kwenda kwa mwajiri wake.

 

Hakika naandika haya huku huzu­ni kubwa ikinigubika, vile ninavyow­aona wanariadha wengine hapa na bendera za nchi zao najiuliza tume­kumbwa na nini Tanzania.