
MWENYEKITI wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na viongozi wengine watano wa chama hicho wamefikishwa katika Mahakama ya Kisutu na kusomewa mashtaka manane ikiwemo kufanya maandamano yaliyosababisha kifo cha Mwanafunzi wa Chuo cha NIT, Akwilina Akwiline, Feb 16 mwaka huu.
Watuhumiwa hao wamesomewa mashtaka hayo na Wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri ambapo Nchimbi amedai kuwa kosa la kwanza ni kufanya mkusanyiko ama maandamano yasiyo na uhalali.
Washtakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa Februari 16, 2018 wakiwa Barabara ya Mkwajuni Dar walikusanyika ili watu waliokuwepo eneo hilo waogope kuona maandamano ya kuvunja amani.
Kosa la pili; Kufanya mkusanyiko usio halali; Wanadaiwa Februari 16, 2018 katika Barabara ya Kawawa, Kinondoni Mkwajuni kwa pamoja wakiwa na watu wengine 12 ambao hawajafikishwa mahakamani wanadaiwa wakati wakiandamana na mkusanyiko wa vurugu waligoma kutii amri ya kusambaratika hali iliosababisha kifo cha Akwilana Akwilini na majeraha kwa maofisa wa Polisi.

Kosa la tatu; Kuhamasisha chuki kwa wanajamii isivyo halali; Mbowe anakabiliwa na tuhuma hizo ambapo anadaiwa Februari 16, 2018 akiwa Viwanja vya Buibui Kinondoni akihutubia wakazi wa maeneo hayo alitoa matamshi ambayo yanadaiwa yangesababisha chuki kwa Jamii, alitoa matamshi ambayo yanadaiwa yangesababisha chuki katika Jamii, alitoa maneno ambayo yangesababisha uasi, alitoa matamshi ambayo yangepandikiza chuki na dharau kwa wananchi wa Tanzania dhidi ya uongozi uliopo madarakani, aliwashawishi wakazi wa maeneo hayo na DSM kutenda kosa la jinai.
Katika kosa linalomkabili Msigwa, Wakili Nchimbi amedai ni kushawishi raia kutenda kosa la jinai ambapo anadaiwa Februari 16, 2018 katika viwanja vya Buibui aliwashawishi wakazi wa maeneo hayo kutembea mbele ya umma wakiwa na silaha.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa wote walikana ambapo Wakili Nchimbi amedai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na anaomba tarehe kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali. Nchimbi aliwasilisha maombi kwa mahakama hiyo ili washtakiwa wasipee dhamana kwa sababu ya usalama wa umma wa Watanzania.