
NENO Video Vixen lina tafsiri kubwa katika sanaa ya muziki hasa wa Hip Hop. Kwa neno jepesi, Video Vixen ni mwanamitindo anayetokea ‘kuonekana sana’ katika video za Muziki wa Hip Hop.
Video Vixen anaweza kuwa muimbaji, dansa au muigizaji. Ipo mifano mingi na wanamuziki wengi duniani ambao wanatambulika kama video vixen na wakati huohuo ni wanamuziki. Wakali hao ni Nicki Minaj, Trina, Eve, Rasheeda, Foxy Brown, Remy Ma, Da Brat, Jacki-O, Shawnna, Gangsta Boo, Angel Haze, LoLa Monroe, Blac Chyna pamoja na Amber Rose.
Kibongobongo, Video Vixen hachagui aina ya muziki, wapo wanaotokelezea kwenye Muziki wa Hip Hop na wengine R&B. Ukiambiwa utaje kati ya ma Video Vixen waliojipatia umaarufu mwanzoni kabisa kwenye tasnia ya Bongo Fleva huwezi kumuacha Agnes Gerard ‘Masogange.’
Katika tasnia ya burudani imepatwa na msiba usioelezeka kwa kuondokewa kwa Video Vixen huyu aliyekuwa akitumika katika video za Kibongo hadi kupelekea kubadilishwa jina na kuitwa Masogange.
Masogange amefariki dunia, Ijumaa iliyopita (Aprili 20) katika Hospitali ya Mama Ngoma, Mwenge jijini Dar akisumbuliwa na Ugonjwa wa Nimonia pamoja na upungufu wa damu. Katika makala haya, yanaeleza kati ya video zake za kukumbukwa alizowahi kubamba nazo;
My Lady – Suma Rider
Kama ulikuwa hujui, hii ni video ya kwanza kabisa ya Masogange iliyomtambulisha katika soko la Video Vixen. Katika video hii ambayo audio ilifanyika Souncrafters huku kideo chake kikisimamiwa na Adam Juma wa Visual Lab, Masogange anaonekana akicheza muda wote na na wakati mwingine akiongozana na Suma Rider.
Ukiangalia kwa makini utaona mwili wa Masogange wa kipindi kile ambapo anaonekana mwembamba sana na pia mweusi huku ‘pamba’ za kizamani zikimpendezesha.
Nangoja Ageuke – AY & FA
Ukiitazama video hii utatamani video vixen wake ageuke tu umuone japo sura yake kwa jinsi alivyokuwa na umbo zuri lililokuwa likimdatisha AY na FA. Kama ulikuwa hujui, video ya Nangoja Ageuke ya MwanaFA akishirikiana na AY, video vixen aliyetumika ni Masogange. Audio ilifanywa na Harmy B huku video ikisimamiwa na wakali kutoka Kenya, Ogopa Video.

Masogange – Belle 9
Baada ya kutamba na wimbo wa Sumu ya Penzi, Belle 9 aliingia studio za Rock Star mkoani Morogoro na kutengeneza wimbo aliouita Masogange. Hakuwa akijua kama utakuja kulitengeneza jina la mtu na kufika nalo mbali.
Ni video za kwanza kwanza kuonekana Masogange iliyopikwa na Adam Juma wa Visual Lab ambapo kioo chake kinamuonesha bi’dada huyo akiwa katika mapozi ya kimahaba na Belle 9 mwanzo mpaka mwisho wa video.Tangu video hiyo ilipotoka na ndio jina la Masogange lilipoanzia.
Msambinungwa – Tunda Man
Katika video hii, ya Khalid Ramadhan ‘Tunda Man’ akimshirikisha Ali Kiba, Masogange aliipendezesha kwa kiasi kikubwa kutokana na kuwa mhusika aliyeonekana akiwagonganisha wanaume (Kiba na Tunda Man). Video ilichukuliwa Mombasa, Kenya pamoja na Dar es Salaam chini ya Dairekta Abby Kaz.
Magubegube – Barnaba
Ni miongoni mwa video alizozing’arisha Masogange akicheza kama mwanamke mcharuko ambapo alikuwa akiishi na mumewe, Mpoki lakini muda huohuo akaanzisha penzi na mchekeshaji, Mboto na mwisho wa siku alifumaniwa.
Kampa – Reggy The Best
Rey hakuwa akifahamika kivile lakini uwepo wa Masogange katika video hii ulimfanya kuibuka na kuanza kufuatiliwa katika Muziki wa Bongo Fleva. Kampa au ukipenda waweza kuiita Kampa Kampa Tena ni bonge moja la video kutoka Reggy akiwa amemshirikisha Rapa Kimbunga Mchawi. Katika video hii, Masogange anaonekana kama demu mwenye kuwachomolea nje wanaume wengi na mwisho wa siku anamkubalia yule wa kwanza kabisa ambaye ni Reggy. Video imesimamiwa na Dairekta Hanscana.
MAKALA: ANDREW CARLOS