
IMEFICHUKA! Kufuatia madai ya kuwepo kwa balaa la maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) katika ulimwengu wa mastaa wa Bongo, kumekuwa na mbio nyingi za kwenda kupima huku nyuma kukiwa na siri nzito, Ijumaa linafunguka.
LIFE STYLE INAWAMALIZA
Kabla ya yote, uchunguzi wa gazeti hili wa muda mrefu ulibaini kwamba, mfumo wa maisha (life style) ya baadhi ya mastaa hao wa kujiachia kwa starehe na anasa zilizopitiliza kama ulevi, kubadilishana wapenzi na mengineyo, yamekuwa yakiwaingiza baadhi yao kwenye hofu kubwa ya kuambukizwa ugonjwa huo.
Ilibainika kwamba, kwa wale wa kike wamejikuta wakinyoosheana vidole kuwa f’lani ana Ukimwi kutokana na tabia yao iliyoshamiri ya kuporana wanaume.

WAKIRI KUIBIANA MABWANA
Wengi wa waliozungumza na gazeti hili walikiri kuwa na tabia ya kuibiana mabwana, jambo ambalo limewaweka kwenye hatari ya kupukutika kama kuku kwa ugonjwa huo hatari wa Ukimwi.
Wapo mastaa wakubwa waliokiri kushiriki ‘kamchezo hako ka’ kushea mabwana na wakati mwingine hata bila kutumia kinga (kondomu).
Wenyewe wanasema baadhi yao ni malimbukeni kwani wakiona mmoja wao amepata bwana mpya anayempa maisha mjini, wote hujikuta wakimmezea mate halafu kummendea mwanaume huyo na kumchukua.

HOFU NA KUKIMBILIA KUPIMA
Ilielezwa kuwa, baada ya hapo, inapotokea kukawa na uzushi au tetesi kuwa ana VVU au Ukimwi au Ngoma, basi walioshiriki mchezo huo hukumbwa na hofu hivyo kulazimika kukimbilia kupima Ukimwi na kama kweli wangekuwa wanatoa majibu sahihi wanayokutana nayo, hakuna atakayepona.
Mmoja wa mastaa hao wakubwa aliling’ata gazeti hili sikio kwamba, hali ni mbaya kwani kiwango cha maambukizi kinaweza kuwa ni zaidi ya asilimia hamsini na ndiyo maana wengi wakipima hutaka kujisafisha kwa kuanika majibu ambayo hakuna mwenye uhakika kama ni kweli au ni ya kutengeneza.
HOSPITALI MAARUFU KWA VYETI FEKI
Hata hivyo, uchunguzi huo ulibaini kwamba, zipo hospitali na vituo vya afya vinavyotoa vyeti halali, lakini zipo baadhi ya hospitali na vituo vya afya ambavyo ni maarufu jijini Dar kwa kutengeneza vyeti vya Ukimwi (tunalifanyia kazi jambo hilo kwa undani).

SIRI YA KWANZA
Kwa mujibu wa msanii mmoja mkubwa wa sinema za Kibongo aliyeomba hifadhi ya jina alidai kuwa, kwanza wengi huamua kupima baada ya kuwepo kwa manenomaneno mitandaoni hivyo kutaka kuweka upepo sawa.
“Na mara zote vyeti vya wanaopima baada ya kuwepo kwa tetesi kuwa wana ngoma, majibu huwa ni HIV-NEGATIVE (yaani hawana).
“Hakuna aliyewahi kuanika majibu yake na kusema anao ndiyo maana kunakuwa na walakini kwenye majibu hayo,” alisema staa huyo na kuongeza:
“Kwa mfano kuna yule… (anatajwa mwanaume aliyefariki dunia) wa Zanzibar. Baada ya kifo chake kila mtu alikuwa na kihoro maana nasikia walikuwa wamepokezana wengi kwelikweli.
“Pia kuna msanii mkubwa wa muziki naye zilienea tetesi kwamba ameungua, kukawa na hofu mpaka ukikutana na mtu unamuona kabisa hana amani moyoni mwake. Lakini hawana wa kumlaumu kwa sababu waliponzwa na tamaa zao.”
SIRI YA PILI
Uchunguzi huo pia ulibaini kwamba, baada ya kupitapita kwenye kashakashi za wanaume wengi kisha kutajwa kwenye mitungo, wengi huamini kuwa, wakipima watawaaminisha wanaume kuwa wako safi ili waolewe.
“Ukiona umri umekwenda na hakuna mwanaume anayekuja wa maana, lazima ufanye kila jambo kuonekana msafi hivyo kupima ni ishu ndogo sana tunapotafuta mume,” alisema mmoja wa mastaa hao kwa sharti la kutotajwa gazetini.
USHUHUDA WA LUNGI
Kwa upande wake, mrembo ambaye pia ni msanii wa sinema za Kibongo, Lungi Maulanga alikiri kwenda kupima ngoma na kuweka majibu yake hadharani ili kumwaminisha mumewe kuwa yupo salama.
“Nilibaini mwanaume wangu alikuwa ana wanawake wengi na kuwa na hofu juu ya maisha yangu kuwa huenda nilikuwa nimeambukizwa ngoma.
“Kweli siku moja nilikwenda kupima na nikapewa majibu kuwa sina, lakini nilipokaa muda mrefu niliamua kwenda kupima tena na nilikwenda kupima kwenye hospitali ya Serikali ya Mwananyamala (Dar).
“Majibu ya Mwananyamala kuwa sina Ukimwi, kiukweli yameniweka huru sana na yamenisaidia kuondoa hofu na kupuuza manenomaneno ya mitaani,” alisema Lungi.
Baadhi ya mastaa ambao walishapima Ukimwi kisha kuanika majibu yao kuwa wako HIV-NEGATIVE (hawana Ukimwi) ni pamoja na Wema Isaac Sepetu, Irene Pancras Uwoya, Elizabeth Michael ‘Lulu’, Maimartha Jesse ‘Mai’, Isabela Mpanda ‘Bella’, Salma Jabu ‘Nisha’ na Lulu Mathias Semagongo ‘Anti Lulu’
Wengine ni Tunda Sebastian, Gift Stanford ‘Gigy Money’, Tamrinah Poshi ‘Amanda’ na Lungi.
HALI YA UKIMWI IKOJE?
Kwa Mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), karibia watu milioni 35 wanaishi na VVU na kati ya hao milioni 1.5 ni watoto walio chini ya umri wa miaka 15.
Inasadikiwa kuwa wengi wa waathirika wa VVU wapo Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Mpaka sasa karibia watu milioni 19 wameshafariki dunia tangu ugonjwa huo ulipoanza kuua miaka 1980.
MASUPASTAA WALIOKUFA KWA UKIMWI DUNIANI
Baadhi ya masupasta wakubwa duniani waliofariki kwa Ukimwi na kutangazwa hadhani kuwa wamekufa kwa ugonjwa huo ni pamoja na Rock Hudson ambaye alikuwa staa wa filamu wa Hollywood nchini Marekani aliyefariki mwaka 1985.
Wengine ni Erick Wright ‘Eazy-E’ ambaye alikuwa prodyuza wa muziki nchini Marekani aliyefariki dunia mwaka 1995, Kevin Peter Hall ambaye alikuwa mwigizaji nchini Marekani aliyefariki dunia 1991 na Freddie Mercury ambaye ni mwanamuziki wa Kitanzania aliyezaliwa Zanzibar aliyefariki dunia mwaka 1991.
NENO LA IJUMAA KWA MASTAA
Gazeti hili kwanza linachukua nafasi hii kuwapongeza mastaa wanaojali afya zao kwa kuweka utaratibu wa kila wakati kwenda kucheki afya zao.
Pili, linawashauri mara wanapobaini wako salama, kutulia na mpenzi mmoja muaminifu kwani kuwapanga wanaume msururu ni kujiweka kwenye mazingira hatarishi kiasi kwamba ukianza kukonda tu unaweza kuhisi unao kumbe hamna kitu.
Tatu, wakati mwingine badala ya kuanika tu majibu ya vipimo vyao vya HIV kwenye mitandao ya kijamii na magazetini, ni vyema kuchukua waandishi na kuongozana nao kwenye zoezi hilo la upimaji ili kujenga imani ya majibu hayo ya NEGATIVE.
Nne, watakaoenda kupima na kubaini wameathirika, wasisite pia kutupa taarifa ili kutoa fundisho kwa watu wengine.
STORI: MWANDISHI WETU, DAR