
MSANII maarufu wa vichekesho ambaye ni miongoni mwa wasanii waliokuwa wakiunda Kundi la Orijino Komedi, Mac Regan Kipara ‘Chura’, amesema kundi lao halijavunjika bali wameamua kupeana nafasi kwa kila mmoja wao kufanya mambo yake binafsi.
“Kundi letu halijavunjika, mtakumbuka tumefanya kazi kwa zaidi ya miaka kumi tukiwa pamoja tena bila kupumzika, hivyo tumeamua kila mmoja wetu afanye mambo yake binafsi kwanza, mimi kwa upande wangu ninajihusisha na kilimo.
“Nina trekta langu ambalo linanisaidia katika masuala ya kilimo ambacho kinaniweka mjini kwa sasa. Lakini siwezi kufuatilia wenzangu wanafanya nini. Mashabiki wajue ipo siku hata kama ni uzeeni tutarudi na kufanya kazi pamoja na kuwaletea kitu kingine kizuri zaidi,” alisema Mac Regan.
Akizungumzia ugonjwa unaomsumbua msanii mwenzake, Vengu, Mac Regan amesema hayo ni masuala ya kifamilia, hivyo hawezi kuyazungumzia kwani hata ripoti za ugonjwa hupelekwa kwenye familia. Aidha, amesema wao kama wasanii na marafiki wa Vengu wanaendelea kumjulia hali kwa kumtembelea na kuwasiliana na ndugu zake.