
MWADUI FC kesho Jumapili itakuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Kambarage pale Shinyanga kuvaana na Yanga lakini imetamka kuwa wanataka heshima hivyo ni lazima washinde mchezo huo.
Yanga imefungwa mechi mbili zilizopita ikiwa ugenini huku presha ikionekana kuwa kubwa katika kusaka kumaliza ligi wakiwa nafasi ya pili. Kwa sasa Yanga wapo nafasi ya tatu na pointi zao 48, Azam wa pili na alama zao 52. Mechi ya mwisho kati ya Yanga na Mwadui iliyopigwa jijini Dar timu hizo zilitoka suluhu.

Yanga ilifungwa dhidi ya Prisons mabao 2-0 kisha ikachapwa na Mtibwa bao 1-0 leo watacheza tena ugenini na Mwadui FC.
Katibu wa Mwadui, Ramadhan Kilao, ameliambia Championi Jumamosi kuwa, licha ya kuwa mchezo utakuwa mgumu, wao wamejiandaa kushinda ili wamalize ligi wakiwa kwenye nafasi za juu lakini pia wanataka heshima kwenye uwanja wao wa nyumbani.
“Tunawaheshimu Yanga kwa sababu ni timu kubwa lakini hatutakuwa tayari kuona tunakosa pointi tatu, tunataka kulinda heshima yetu kwani ukiangalia mechi ya mzunguko wa kwanza tulitoka suluhu, hivyo tunahitaji ushindi ili tuwe wababe wao,” alisema Kilao.