×

Usajili Ufanyike Kwa Ufundi, Siyo Kukomoana

 TAYARI hekaheka za usajili kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara zimeshaanza, huku baadhi ya timu zikiwa zimesha­fanikiwa kuwapata wachezaji wao wapya.

 

Lengo kubwa la usajili kawaida huwa ni kuboresha kikosi ili kiwe na ushindani wa kutosha katika msimu husika, lakini bahati mbaya usajili wa timu nyingi za Kibongo umekuwa na tafsiri tofauti.

 

Klabu nyingi, zimekuwa zikisajili kwa ajili ya kuwakomoa wapinza­ni lakini ile dhana ya kuboresha kikosi, imekuwa ni aghalabu sana kukuta ikitumika kwa klabu nyingi.

 

Wengi, wanaposikia mchezaji fu­lani anawaniwa na timu fulani pin­zani, hapohapo nao wanarusha ndoano, bila hata kujali mahitaji yao, matokeo yake kunakuwa na mrundikano wa wachezaji kwenye kikosi kimoja, ambao hata hivyo, hawapati nafasi ya kucheza.

 

Championi tunaamini kwamba kla­bu zinatakiwa kufanya usajili, lakini tunasisitiza kuwa usajili huo ufan­yike kwa kuzingatia mahitaji ya timu na kwa maelekezo ya benchi la ufundi.

 

Usajili wa kukomoana hauna tija, mwisho wa siku timu inaweza ika­jikuta imerundika wachezaji wen­gi lakini wasio na mchango katika timu, unakuwa ni usajili wa ‘bora liende’.

 

Wakati usajili ukiendelea, tungependa kuzishauri klabu kwamba zinatakiwa ziwe ma­kini katika usajili na kwamba zisajili kwa kutumia busara, hekima na kwa kuzingatia ma­hitaji yao, siyo suala la kuko­moa.

Bodi ya Uhariri/Maoni