
UONGOZI wa Yanga unaendelea kufanya usajili kimyakimya na umakini mkubwa kwa ajili ya kuimarisha kikosi chao ambapo wamepanga kuwatambulisha wachezaji wote waliowasajili ijumaa ijayo.
Yanga wamesema kuwa watawatambulisha wachezaji hao siku hiyo kwa kuwa ndiyo usajili utakuwa umefunguliwa.
Timu hiyo hivi karibuni ilitangaza kufanya usajili wa kimyakimya kwa hofu ya wapinzani Simba na Azam FC na Azam FC kuwazidi ujanja na kuwasajili kama ilivyokuwa kwa Adam Salamba, Habib Kiyombo, Marcel Boniventure na Mohamed Rashid waliokuwa wanawawania Yanga.
Yanga hadi sasa tayari imefanikiwa kumbakisha beki wao mkongwe, Kelvin Yondani aliyekuwa anawaniwa na Simba, huku ikielezwa kumsajili mshambuliaji mpya Mbenin, Marcelin Degnon Koupko na beki raia wa Ivory Coast, Pascal Wawa.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa alisema tayari imemalizana na baadhi ya wachezaji kwa kusaini mikataba ambao majina ni siri.
“Klabu zinavyofanya usajili kwa hivi sasa zinakiuka kanuni kwa kuwa dirisha la usajili bado halijafunguliwa.
“Lipo wazi hilo, klabu zinazosajili hivi sasa zinaenda kinyume na utaratibu wa usajili na hiyo ni kutokana na dirisha la usajili kutofunguliwa.
“Sisi kama Yanga tumepanga kuwatambulisha usajili wa wachezaji wetu wapya baada ya dirisha la usajili kufunguliwa na tumepanga kufanya usajili kutokana na mapendekezo ya kocha ambayo ameyatoa kwa uongozi.
“Mashabiki na Wanachama wetu wa Yanga wavute subira, muda ukifika kila kitu tutakiweka wazi kwa maana ya kutangaza usajili wa wachezaji tuliowasajili,” alisema Mkwasa.
Stori: Wilbert Molandi, Championi
