WIKIENDI iliyopita timu ya Simba ilichapwa mabao 2-0 na Gor Mahia ya Kenya katika mchezo wa fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup iliyofanyoka Nakuru, Kenya.
Simba ilishindwa kufurukuta mbele ya wenyeji Gor Mahia katika Uwanja wa Afraha nchini Kenya ilipofanyika michuano hiyo kutokana na kutokuwa vizuri kwenye safu yao ya ushambuliaji, hivyo kuwapa nafasi wapinzani wao hao kuibuka na ushindi.
Safu ya ushambuliaji ya Simba kiujumla haikuwa nzuri kutokana na kuwakosa washambuliaji wake mahiri, John Bocco na Emmanuel Okwi hivyo kusababisha safu hiyo kuwa butu kutokana na kushindwa kufunga bao hata moja tangu michuano ilipoanza hadi walipofikia hatua ya fainali ambapo walifanikiwa kutinga hatua hiyo kupitia mikwaju ya penalti.
Michuano hii ilikuwa na hamasa kubwa hasa kutokana na kufahamika kuwa bingwa wa michuano hiyo anapata nafasi ya kukwea pia kwenda nchini England kucheza mchezo wa kirafiki na Everton.
Ukiachana na Simba timu zote za Tanzania ambazo zilishiriki michuano hiyo, ikiwemo Yanga na Singida United zimeshindwa kufurukuta katika michuano hiyo kutokana na kufanya vibaya ambapo Yanga ilitolewa katika hatua ya kwanza na Singida wakimaliza wa tatu.
Inaonyesha wazi kuwa klabu zetu hazijaichukulia michuano hii kwa umakini wa hali ya juu kutokana na matokeo ambayo wameyapata.
Yanga na Simba zote zilionekana kuwatumia zaidi wachezaji wapya na wale wa vikosi vya pili hali iliyowafanya watoke mapema kwani wengi wao walionekana hawana uzoefu wala muunganiko kwenye timu husika.
Hali hiyo imeonekana kujirudia katika michuano ya msimu huu ambapo kikosi cha Simba kimewaacha washambuliaji wake tegemeo ambao ndio walioiongoza timu hiyo kuchukua ubingwa kwa kufunga mabao 34 kwa pamoja jambo ambalo si sahihi.
Sikatai kwamba Gor Mahia ni timu nzuri na ina ushindani mkubwa, lakini naamini uwepo wa wachezaji hao kungeongeza ushindani zaidi na hata kufanikiwa kushinda ili kuweza kuipata nafasi ya kwenda nchini England.
Kama wachezaji hao waliachwa kutokana na kuwa majeruhi ambao matatizo yasiyozuilika, hilo halina jinsi hata kidogo ila iwapo waliwaacha tu kwa sababu ya kuwapumzisha ili kutumia zana mpya haikuwa sahihi kwani uongozi ulipaswa kutambua umuhimu wa michuano hiyo kwa kutoibeza hata kidogo.
Walitakiwa kuichukulia umakini wa hali ya juu michuano hii ili kuweza kujiimarisha zaidi kwa kuwa na kikosi imara na si kuifanya michuano hiyo kuwa sehemu ya kupimia wachezaji wapya ama wale ambao walikuwa hawapati nafasi.
Ikumbukwe kuwa, kupata nafasi ya kucheza na Everton tena kwao ni sehemu ya kujitangaza kwa klabu na nchi kwa ujumla hivyo kuikosa nafasi hiyo ni jambo la kusikitika sana.
Kila kukicha tumekuwa tukilalamika juu ya soka la Tanzania kutosonga mbele na badala yake hurudi nyuma kila kukicha hivyo nafasi kama hizi zitumike katika kupiga hatua.
Viongozi wanapaswa kujilaumu kwa maamuzi waliyoyafanya ya kutowatumia wachezaji hao ambao walionyesha kiwango msimu mzima kulikochangia timu kutwaa ubingwa kutokana na kuchukulia mambo kirahisi rahisi.
Acha Niseme na KHADIJA MNGWAI
Comments are closed.