
BAADA ya ukimya wa muda mrefu wa mzazi wa staa wa Bongo Fleva, Ally Salehe Kiba, mzee Salehe hatimaye Ijumaa limemuibua na kujua mambo mbalimbali yanayomhusu ambayo yalikuwa hayajulikani.
Tofauti na wasanii wengine ambao wamekuwa wakiwaanika wazazi wao na mashabiki wao wakiwajua, kwa Kiba ilikuwa ni vigumu sana kumuanika mzazi huyo wala watu kujua habari zake.
Kutokana na ukimya huo, mitandaoni yalisemwa mengi kumhusu mzazi huyo huku wengine wakidai huenda labda ni mgonjwa sana, wengine wakisema Kiba amemzuia asionekane.

KIBA AMTUPIA KIAINA
Baada ya ukimya wa miaka mingi, hivi karibuni katika Siku ya Wababa Duniani, kupitia ukurasa wake wa Instagram, Kiba alitupia picha ya mzazi wake huyo kiaina bila kuainisha kama ndiye baba yake.
Katika ‘posti’ hiyo, Kiba aliweka picha mbalimbali za kwake pamoja na ya baba yake huku akisindikiza na ujumbe wa kuwatakia mashabiki wake siku njema ya Wababa.
IJUMAA LAMSAKA
Baada ya kusemwa mengi juu ya ukimya wa baba yake Kiba, Ijumaa liliamua kumfungia kazi ili kuweza kumuona na ikiwezekana kuzungumza naye.
Lengo si baya; bali kujibu maswali ya wadau wa familia hiyo ambayo imetoa mwanamuziki nguli nchini yanayoulizwa kila mara:
“Hivi baba wa Alikiba kwa nini huwa haonekani kwenye vyombo vya habari na kwenye mitandao ya kijamii akimsapoti chochote mwanaye?”
NI MUHEZA KARIAKOO
Katika uchunguzi wake, Ijumaa liliweza kupafahamu nyumbani wanakoishi wazazi wa Kiba, Kariakoo Dar, Mtaa wa Muheza na kubaini mambo mengi yanayomhusu mzee huyo na familia yake ambayo ni tofauti na fununu za mitandaoni.
Licha ya kufanikiwa kuwakuta wazazi wote wawili wa Kiba, Ijumaa liliweza kuzungumza na dada yake Kiba aitwaye Zabibu Kiba aliyeomba azungumze kwa niaba ya wazazi hao wakiwa wanasikiliza ambapo alifichua siri iliyofichwa kwa miaka mingi ya kwa nini mzee huyu amekuwa hajitokezi hadharani kama wenzake.
NI WATU WA DINI
Katika nyumba hiyo wanayoishi mzee Salehe, Zabibu na mama yao, Ijumaa lilibaini mzee huyo pamoja na familia yake ni watu wenye kushika dini sana ya Kiislamu na wanaofuata misingi halisi ya imani hiyo.
KIBA ANAMJALI BABA’KE
Katika kipindi ambacho Ijumaa lilikuwa nyumbani hapo, ilibainika kuwa tofauti na wasanii wengine ambao hawawajali wazazi wao, mzazi wa Kiba alionekana kuwa watoto wake wanamjali.
Zabibu alikuwa na wazazi wake kwa ukaribu huku ikionekana dhahiri Kiba amekuwa akiwahudumia wazazi wake kwani hakukuwa na lawama zozote zilizoelekezwa kwake.
MZEE SI MTU WA ‘MEDIA’
Ijumaa lilibaini kuwa baba yake Kiba si mtu wa mitandao wala vyombo vya habari na ndiyo maana amekuwa haonekani hovyo.
“Hapendi kuonekanaonekana ni maamuzi yake, hivyo tunaheshimu, hatuwezi kufanya tofauti na matakwa yake,” alisema Zabibu.
HAFICHWI
Akizungumzia madai ya kufichwa ambayo yamesambaa kwenye mitandao ya kijamii, Zabibu alisema hayana ukweli bali ni aina ya maisha ambayo mwenyewe ameyachagua.
“Hatujamficha. Ni maamuzi yake kama nilivyosema lakini hata hivyo, siku mimi nikijisikia kumposti nitafanya hivyo kama alivyofanya Kiba hivi karibuni,” alisema Zabibu.
KUHUSU AFYA YAKE
Ijumaa lilimuuliza Zabibu kuhusu afya ya mzee huyo ambaye kitabia ni mpole ambapo alisema hana matatizo makubwa ya kiafya kama ilivyoenezwa mitandaoni bali hali ya uzee wakati mwingine imekuwa ikimdhoofisha.
“Haumwi hivyo wanavyosema yuko hoi, anaishi na mkewe kwa kipindi chote. Ni matatizo ya kawaida kama ambavyo mzee mwingine mwenye umri kama wake anaweza kukabiliana nayo,” alisema Zabibu.
Ijumaa pia lilibaini kuwa, taarifa za kwamba mzazi huyo hakuhudhuria harusi ya Kiba iliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Serena zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii, hazikuwa na ukweli kwani mzee huyo alihudhuria akiwa na afya njema kabisa.
IJUMAA LAANUA VIRAGO
Kutokana na mazungumzo hayo, hadi Ijumaa linaondoka nyumbani hapo lilibaini kuwa mzee huyo anaishi vizuri na familia yake lakini amechagua kuishi maisha ya kutojionesha kwenye vyombo vya habari kama ilivyo kwa wazazi wengine wa mastaa.
WAZAZI WA MASTAA MAARUFU
Miongoni mwa wazazi wa mastaa maarufu ni pamoja na mama na baba yake Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, mama yake Wema Sepetu, mama yake Irene Uwoya na mama wa mwanamitindo Hamisa Mobeto ambao wamekuwa hawakauki kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
STORI: Memorise Richard na Shamuma Awadhi, IJUMAA