×

Dili la Kobe 536 Latibuka

DODOMA: Jeshi la polisi kwa kushirikiana na askari wa idara ya wanyamapori jijini Dodoma wameharibu dili kwa kukamata kobe 536 waliokuwa wakisafirishwa nje ya nchi kupitia Zambia wenye thamani ya shilingi milioni 84.

Baadhi ya mashuhuda walioshuhudia tukio hilo walisema waliona watu wanne wakiwa wametaitiwa na polisi na masanduku yao, lakini walipopekuliwa walikutwa kobe hai kwenye masanduku hayo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, SACP Gilles Muroto alithibitisha kutokea kwa tukio hilo akasema kobe hao ni wa aina mbalimbali na walikamatwa Dodoma ambako ndiko kunakoaminika kuwa ni kitovu cha ukusanyaji wa wanyama hao kutoka sehemu mbalimbali.

“Ni kweli tumekamata wanyamapori hai aina ya kobe 536. Wanyama hao walikuwa wa aina mbili ya pan cake na aina ya leopard wenye thamani ya shilingi 84, 589,400 na katika tukio hilo watu wanne tumewakamata,” alisema Kamanda Muroto.

Naye Ofisa wa Wanyamapori Mkoa wa Dodoma, Silivester Okudo aliwaomba Watanzania popote wanapoona watu wasio wazalendo wanakusanya kobe au vyara nyingine za Serikali bila kibali wawafichue.

“Tunawaomba Watanzania wawafichue watu wanaokusanya kobe au nyara nyingine za Serikali bila kuwa na vibali ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao,” alisema Okudo.

Hii siyo mara ya kwanza Serikali kukamata wanyama hao. Mwaka Novemba 17 mwaka 2015 Jeshi la Polisi Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), liliwahi kuwakamata watu wawili kwa tuhuma za kutaka kusafirisha kobe hai 201 wenye thamani ya Sh 30.4 milioni waliokuwa wanapelekwa Kaula Lumpa, Malaysia.

Aliyekuwa Kamanda wa Polisi JNIA, Martin Otieno alisema kobe hao aina ya Indian Star, waliwekwa watatu hadi sita ndani ya soksi na kisha kwenye pampasi kubwa ndani ya mabegi matano ili kwenye mashine ya ukaguzi isijulikane kilichomo ndani ya mabegi hayo.

STORI: MWANDISHI WETU, UWAZI