
Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), imezindua JUKWAA LA FIKRA litakalokuwa linawakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali na wananchi ili kujadili MADA mbalimbali za kitaifa, KIZALENDO, kwa lengo la KUTAFUTA UFUMBUZI WA PAMOJA kuhusu baadhi ya matatizo na changamoto tunazokabiliana nazo kama nchi.
Jukwaa hilo linalenga kuwaleta pamoja viongozi wa serikali, watunga sera, wadau mbalimbali, jumuiya ya kimataifa na kikanda, watendaji wakuu wa makampuni na mashirika mabalimbali nchini, wanadiplomasia, watalaamu kutoka sekta mbalimbali, wasomi, wanafunzi, waathirika na watanzania wote wanaoitakia mema nchi yetu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Ltd, Francis Nanai, alisema kuwa, lengo kuu ni kuendeleza mjadala wa jinsi ya kukabiliana na changamoto kadhaa zinazoikabili nchi hii na kuathiri mchango katika pato la taifa. Ni la kutafuta suluhisho pamoja siyo kunyoosheana vidole.
Mada ya Kwanza – Alhamisi 28/06/2018:
“Nina furaha kubwa kuwakaribisha nyote kwenye mjadala huu wa kwanza kabisa ya ‘MCL Jukwaa la Fikra’ ambalo utafanyika kesho siku ya Alhamisi tarehe 28/ 6/2018, kuanzia saa 3 kamili mpaka saa 5 usiku. Mada yake ya kwanza – inayosema “Afya Yetu, Mtaji Wetu” – “inalenga kuangalia changamoto zinazotokana na magonjwa yasiyoambukiza nchini, (NCDs), alisema Nanai.

Alifafanua kuwa, wameamua kuanza na mada ya magonjwa yasiyoambukiza kwa sababu ya changamoto zinazotokana na ongezeko la magonjwa haya miongoni mwa Watanzania.
“Tatizo ni kwamba, magonjwa haya hata kama hayajakuathiri wewe moja kwa moja, basi yatakuathiri kupitia kwa wale ulio karibu nao kama familia, ndugu, rafiki au kupitia mzigo wa huduma za afya ambao unabebwa na ama serikali, ama mwajiri, au familia, ambapo hulazimisha kutumia rasilimali chache tulizonazo kukabiliana na magonjwa haya.
“Tukiwa na mjadala wa pamoja wa wadau muhimu wa sekta ya afya na hasa wataalamu wa magonjwa yasiyoambukiza, tuna imani kuwa, Jukwaa litatoa fursa ya wao kuwa na majadiliano ya kina wakiwashirikisha watanzania wengine na kuangalia changamoto na matatizo yaliyopo, lakini muhimu sana ni kupendekeza suluhisho ambalo wanadhani litasaidia kukabiliana na changamoto hizo,” na upande wa serikali na watunga sera kuwa tayari kuyachukua mapendekezo na kuyafanyia kazi, alisema Nanai.
Aliwataja baadhi ya washirika waliowezesha kufanyika kwa uzinduzi wa Jukwaa hilo kuwa ni Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, na Shirika la Afya Duniani (WHO) huku akitoa shukrani za pekee kwa ITV/Radio One, ambao alisema ndio washirika wakuu kwa upande wa habari.

“Tunawashukuru pia wafadhili wetu wakiwamo Mfuko wa Bill & Melinda Gates, Benki ya NMB pamoja Hotel & Club ya Mazoezi ya Colloseum kwa michango yao ya hali na mali katika kufanikisha jukwaa hili. Nina furaha kubwa kuwakaribisha wote na ni matarajio yangu kuwa mjadala wa kesho utatuwezesha kupata ufumbuzi ambao utalisaidia Taifa katika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza (Non-Communicable Diseases, NCDs).
Kitakachofuata Baada ya Mjadala:
“Baada ya mjadala, Jukwaa La Fikra litakusanya pamoja mrejesho utakaopatikana na kuandika ripoti itakayoainisha mapendekezo ya nini kifanyike na kuikabidhi kwa Wizara husika na wadau wengine kwa ajili ya utekelezaji katika maeneo husika,” alisema Nanai.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ITV/Radio One, Bi Joyce Mhaville, aliishukuru MCL kwa ubunifu ambao alisema kuwa ni wa kisasa zaidi na utawapa wananchi na wadau uwanja mpana wa kujadili matatizo yanayowakabili na kupata suluhisho.
“Kwanza niishukuru MCL kwa kuona umuhimu wetu sisi kama ITV/ Radio One kuwepo katika jitihada hizi, lakini pia niwapongeze kwa ubunifu ambao unalenga kuwasaidia watanzania walio wengi na taifa hili kwa ujumla. Ninaamini kuwa jukwaa hili litafikia malengo yake kwa maana ya kufikia kile kinachotarajiwa,” alisema Bi Mhaville.