
UONGOZI wa Klabu ya Yanga umefunguka umafia waliofanyiwa na watani zao Simba, juu ya aliyekuwa mchezaji wa Lipuli FC ya Iringa, Adam Salamba waliyemsajili hivi karibuni.
Simba ilifanikiwa kupata saini ya Salamba kwa dau la Sh milioni 40 ili asaini kuitumikia timu hiyo msimu ujao wa 2018/19 baada ya kuwazidi kete wapinzani wao hao wa jadi.
Akizungumza na ChampionI Ijumaa, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika alisema kuwa, Salamba ndiye mchezaji pekee waliyekuwa wakimuhitaji kati ya wale wote waliowasajili Simba baada ya kuwazidi ujanja.
“Hakuna mchezaji hata mmoja kati ya waliosajiliwa Simba ambao tulikuwa tukiwahitaji, mchezaji ambaye tulikuwa tukimfuatilia na kumuhitaji alikuwa Salamba ambaye tulipeleka hadi barua lakini walikuja kumsajili dakika za mwisho.
“Baada ya kuona hivyo tumeona ni vyema kuangalia upande mwingine kwa kutazama wachezaji wengine kwa kuwasajili na kila kitu kinaenda vizuri na mipango ikikamilika kila kitu kitakuwa sawa,” alisema Nyika na kudai kuwa wengine wote ambao wamesajiliwa na Simba hawakuwa kwenye mipango yao rasmi.