×

TICHA AMFANYIA KITU MBAYA DENTI WAKE

DAR ES SALAAM: Mwalimu mmoja aliyefahamika kwa jina la Rebeca wa Shule ya Sekondari ya Carmel iliyopo Mbezi jijini Dar anadaiwa kumfanyia kitu mbaya mwanafunzi wake wa kidato cha pili (jina linahifadhiwa kwa sababu za kimaadili).

AMEMPA KIPIGO

Mwalimu huyo anadaiwa kumsababishia mwanafunzi huyo wa kike majeraha mengi sehemu mbalimbali za mwili chanzo kikitajwa kuwa ni masuala ya kifamilia ya binti huyo.

Akizungumza huku akiwa kitandani nyumbani kwao Mbezi akiugulia maumivu, mwanafunzi huyo alidai kuwa alipigwa na mwalimu huyo baada ya mama yake wa kambo kwenda kumshitaki shuleni hapo kwamba hana nidhamu kwa kuwa amemtumia ujumbe wenye kukosa adabu.

Akisimulia kwa kirefu mwanafunzi huyo alishusha madai haya mazito hivi: “Mimi ninaishi na shangazi yangu kwa sababu mama yangu mzazi alishafariki dunia kwa hiyo baba yangu ana mke mwingine ambaye anaishi naye.“Mama huyo aliamua kunikomesha kwa kwenda shuleni kunishitaki kwamba namvunjia heshima, ndipo mwalimu akaniadhibu kwa kunipiga.

“Ilikuwa Jumanne mchana, mwalimu aliniita ofisini, nilipofika pale nikamkuta mama yangu wa kambo aitwaye Lidya akiwa amekaa katika kiti, baada ya hapo kuna mwalimu aliniambia mama amekuja kunishitaki kuwa nimemtumia meseji mbaya, bahati nzuri mwalimu mkuu alikuwepo akaziangalia zile meseji akasema, watazungumza na mimi halafu akaondoka.

“Baada ya hapo akaja mwalimu Rebeka akaanza kunipiga fimbo ambazo sikuweza kuzihesabu kwa kuwa nilikuwa naugulia maumivu.“Alinipiga makalioni, mabegani na mapajani, usoni, alinipiga vibao na yule mama yangu alikuwa palepale na akawa anamwambia mwalimu kuwa mimi ninamdharau nikawa namjibu kuwa mimi simdharau.

“Alipomaliza kunipiga, akaniambia nipige magoti, nikapiga magoti akaniuliza; ulikuwa unajua hiyo meseji uliyoiandika ni kama unamtukana baba yako? Nikamwambia mimi sijui kama nimemtukana, akaniambia nenda darasani. “Nilipoinuka akanishika kwenye koromeo akanisukumiza ukutani, akaniambia unajua mimi naweza kukufanya chochote huku akinipiga makofi.

“Akanyanyua fimbo akaniambia lala chini, sasa kwa kuwa makalio yalikuwa yanauma nikawa najifikiria, ndipo akaanza kunipiga mikononi huku akiniambia nimuombe mama msamaha wakati mwanzo nilishamuomba msamaha.”

Alisema baada ya hapo alirudi nyumbani akiwa hoi na ndugu zake walipomuona amevimba mwilini walimuuliza kulikoni na alipowaeleza mkasa nzima ndipo walipogeuka mbogo na kuamua kwenda shuleni Jumatano iliyopita ili kujua kisa kwa undani.

Gazeti hili lilipewa taarifa juu ya msafara huo na kuongozana na ndugu hao, walipofika shuleni na kuomba kuonana na mkuu wa shule, katibu muhtasi wake alisema ametoka na alipompigia simu alielekeza ndugu hao wamuone mwalimu wa taaluma aliyejulikana kwa jina moja la Sylvester, walipomuona mwalimu huyo alisema:

“Kosa lile alilofanya kijana ni la kifamilia na ile adhabu haikustahili hivyo nendeni polisi mpate PF 3 ili akatibiwe. Mwalimu aliyemjeruhi hamuwezi kumuona, nimempa ruhusa kwa kuwa ana matatizo.”

Ndugu hao waliamua kwenda Kituo cha Polisi Mbezi Luis kupata PF 3 ili mtoto apelekwe hospitali kutibiwa kama walivyoshauriwa na mwalimu huyo. Mpaka tunakwenda mtamboni, ndugu hao walikuwa kituo cha polisi kuhakikisha sheria inafuata mkondo wake. Gazeti hili linafuatilia kwa karibu sakata hili.