×

Martial: Familia Kwanza, Man U Baadaye

Anthony Martial

KIUNGO mshambuliaji Anthony Martial ametetea uamuzi wake wa kuchukua muda mrefu kuwa na familia yake kuliko kurejea kwenye majukumu yake ya Manchester United kwa kusema familia ndiyo ya muhimu kuliko kitu kingine.

 

Mchezaji huyo aliondoka kambini wakati timu ikiwa Marekani baada ya mpenzi wake kujifungua mtoto wa kiume, jambo ambalo lilimkwaza kocha wake, Jose Mourinho kutokana na kuondoka bila kumuomba yeye ruhusa.

 

Mourinho alinukuliwa akisema kuwa hajui Martial atarejea lini kazini huku taarifa nyingine zikieleza kuwa klabu yake imempiga faini ya pauni 180,000 kwa kuchelewa kurejea kazini bila kutoa taarifa.

 

Martial, 22, amethibitisha kuwa alitarajiwa kurejea kazini jana Alhamisi bila kujali kuhusu faini aliyokatwa ambayo ni sawa na mshahara wake wa wiki mbili.

 

Akitumia ukurasa wake wa Twitter, nyota huyo aliandika: “Asanteni wote mlionitumia ujumbe, mtoto wangu Swan anaendelea vizuri, mama yake naye yuko sawa japo alipata ugumu lakini namshukuru Mungu kwa sasa afya yake ipo vizuri.

 

“Samahani kwa kuwa familia yangu ndiyo muhimu kwanza… nitarejea kazini Manchester kesho (jana).”

 

Ujumbe huo ni kama mwendelezo wa mvurugano kati ya mchezaji huyo na kocha wake ambaye ni wazi ameonyesha nia ya kutomhitaji kikosini.

 

Mourinho anataka kumuuza mchezaji huyo kabla ya dirisha kufungwa Alhamisi usiku ya wiki ijayo, upande wa Martial aliwaambia rafiki zake wa karibu kuwa hakutaka kurejea kambini wakati timu hiyo ilipokuwa Marekani.