KWA kawaida makocha na wachezaji wengi huwa wanatumia mechi za maandalizi ya msimu kwa ajili ya kuwa kitu kimoja, kufundishana mbinu na hata mechi zinazochezwa hapo huwa siyo zile za kutumia nguvu.
Ikiwa imesalia wiki moja kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu ya England ‘Premier League’, upande wa Manchester United hali ni tofauti, kwa ufupi ni kama upepo umevurugika klabuni hapo.
Mhusika mkuu katika ‘kivuruge’ hicho ni kocha wa timu hiyo, Jose Mourinho ambaye amekuwa akitoa lawama kadhaa juu ya baadhi ya mambo kutokwenda sawa.
United iliamua kwenda Marekani kufanya ziara hiyo ya kujiandaa na msimu, lakini inavyoonyesha wazi Mourinho hana uhusiano mzuri na bosi wake, Ed Woodward ambaye ni makamu mwenyekiti kuhusu sera ya usajili.
Mourinho ameweka wazi kutofurahishwa na usajili uliofanyika, alinukuliwa akisema alitoa mapendekezo yake ya wachezaji anaowahitaji na anahisi hatawapata wote anaowahitaji.
Wakati dirisha la usajili likitarajiwa kufungwa usiku wa Alhamisi ijayo Agosti 9, Mourinho amekuwa akiwatolea kauli kali wachezaji wake hadharani kiasi cha kuaminika kuwa hawana furaha na aina ya ukosoaji wake huo.
Baadhi ya mambo ambayo amekuwa akilalamika ni ratiba ya mechi za kirafiki kuwabana, wachezaji wake kutokuwa fiti, kukosa wachezaji wa kikosi cha kwanza na kuwalaumu viongozi wake kwa kutotimiza usajili anaohitaji.
Huu ni uchambuzi wa kukumbusha wachezaji wa United ambao wametolewa kauli tata kutoka kwa Mourinho ambaye alimaliza msimu uliopita akiwa hana taji lolote.
MOURINHO VS ANTONIO VALENCIA
Hii imewashangaza wengi kwa kuwa mkongwe huyu hana kawaida ya kukwaruzana na makocha wake tangu aanze kucheza soka la kulipwa.
Alimkosoa beki wake wa kulia, Valencia kuwa hakuwa fiti, alirejea kutoka likizo akiwa hana mazoezi na ndiyo maana akaumia kirahisi.
“Nafikiri Antonio Valencia alikuwa na likizo ndefu kwake, hakuwa na hali nzuri, baada ya muda akaumia,” alisema Mourinho baada ya United kuchapwa 4-1 na Liverpool.
Kuumia kiazi cha mguu kwa Valencia kutamfanya kukosa mechi ya ufunguzi wa Premier League dhidi ya Leicester City.
MOURINHO VS ANTHONY MARTIAL
Msimu uliopita alikuwa akimpa nafasi mara kadhaa, alipoona hajafikisha ubora anaouhitaji akaanza kumpiga benchi, hivi karibuni uhusiano wao unaonekana kuzidi kulegalega.
Martial aliondoka kambiini kurejea Ufaransa ambako mpenzi wake alijifungua, Mourinho hakufurahia hilo na akanukuliwa akisema kuwa hakutoa baraka za safari hiyo.
Mbali na hapo Mourinho amekuwa akimkosoa mara kadhaa Mfaransa huyo kiasi cha kumfanya aanze kutafuta mlango wa kutokea.
“Anthony Martial amejaaliwa kupata mtoto, baada ya kuhakikisha ana afya njema alitakiwa kumshukuru Mungu na kurejea kazini, lakini hadi sasa hajarudi na sijui kwa nini,” alisema Mourinho.
MOURINHO VS CHRIS SMALLING/PHIL JONES
Msimu wa 2016-17, Mourinho aliwakosoa walinzi wake hao wa kati kwa kuwa na sababu nyingi za kutofanya vizuri. Hata walipoumia walikaa muda mrefu nje jambo ambalo lilimkera kocha huyo.
MOURINHO VS LUKE SHAW
Mchezaji ambaye ameongoza kwa kukosolewa na Mreno huyo ni Shaw ambaye ni beki wa kushoto, amekuwa akisemwa na kocha huyo kuwa ni mzito, hajitumi, mgumu kuelewa na mambo mengine kama hayo.
Mourinho amekuwa hafichi hisia zake kwa kumkosoa mchezaji huyo hadharani. Mbali na hapo aliwahi kulalamika kuwa akiumia kidogo anashindwa kucheza na kuomba udhuru.
Kuna wakati alitoa kauli hii: “Ni vigumu kumuweka Shaw hata benchi tu kwa kuwa siwezi kumfananisha na Ashley Young, (Matteo) Darmian na (Daley) Blind.”
MOURINHO VS HENRIKH MKHITARYAN
Mourinho ndiye ambaye alimsajili lakini baadaye alioona anashindwa kufanya kile anachotaka, ikabidii amuuze kwenda Arsenal.
“Sikufurahishwa na kiwango chake, sizungumzii mechi moja au mbili bali ni nne au tano, alianza msimu vizuri lakini baada ya muda akawa anarudi nyuma katika ufungaji na hata kutoa asisti, hakuwa vizuri katika majukumu yake ya namba kumi,” alinukuliwa Mourinho.
MOURINHO VS PAUL POGBA
Hapa ndipo shughuli ipo, Mourinho alimsajili kwa pauni 89m na kuweka rekodi wakati huo ya kuwa mchezaji ghali zaidi kusajiliwa duniani.
Baada ya kutwaa ubingwa wa dunia, wengi walitegemea Mourinho atamsifia staa wake huyo lakini kauli alizotoa kuhusu Pogba zilionyesha wazi kuna mambo hayako sawa.
Msimu uliopita alimkosoa mara kadhaa Pogba hadharani kiasi cha kuamua kumpiga benchi katika mechi kadhaa.
MOURINHO VS MARCUS RASHFORD
Mwishoni mwa msimu uliopita baada ya United kufungwa bao 1-0 na Brighton, Mourinho hakufurahishwa na kiwango cha Rashford ambaye alipewa majukumu ya kushambulia lakini akajikuta akikosa nafasi nyingi za wazi.
“Kwa nini Lukaku kila siku? Naamini mmeona sababu, wanashindwa kuonyesha uwezo binafsi, wachezaji wanaopewa nafasi badala ya wengine wanashindwa kuonyesha ukali wao na hawapo katika levo inayotakiwa,” alisema Mourinho akimlenga Rashford.
Comments are closed.