×

MKE ASIMULIA MUMEWE ALIVYOUAWA KINYAMA

DAR ES SALAAM: Katika hali isiyokuwa ya kawaida na kushtua, familia ya Silayo imegubikwa na majonzi mazito tangu walipompoteza ndugu yao Gaudance Alphonce Silayo ‘Bwana Shee’ kwa kifo cha kutekwa na watu wasiojulikana kisha kuuwa kinyama kwa kuchinjwa shingo na kutobolewa macho kisha wauaji hao kuondoka na pikipiki mpya aina ya Boxer.

Gazeti la Amani lilifika maeneo ya Mbezi Makabe jijini Dar ambako alikuwa akiishi marehemu enzi za uhai wake huku akishughulika na udereva wa bodaboda katika Kituo cha Mbezi Mwisho na kukutana na mke wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Gisela Charles Kimario aliyetoa simulizi nzito ya mumewe.

Alisema mwanzoni wa mwezi wa pili mwaka huu, mumewe alinunua pikipiki aina ya Boxer toleo jipya ambayo alianza kufanya nayo kazi ya bodaboda. Hata hivyo, alisema hivi karibuni mumewe mauti yalimkuta baada ya kukodiwa na watu wasiojulikana na kumpeleka kusikojulikana kisha kumuua na kumpora pikipiki.

“Siku hiyo mume wangu aliondoka nyumbani kwenda kazini kwake mimi niliendelea na majukumu ya kawaida ya kuwaandaa watoto kwenda shule, saa zikaenda hadi giza likaingia. “Siku hiyo alikuwa amewasiliana na mimi mara moja tu mchana alipouliza kama watoto wake wamekula. Ratiba ya kurejea kwake nyumbani huwa ni saa tano usiku imezidi sana saa sita.

“Kama ikitokea kupitiliza muda huo mume wangu alikuwa na tabia ya kunipigia simu na kunieleza kwamba atachelewe kurudi,” alisema Gisela. Aliongeza kuwa siku hiyo mambo yalikuwa tofauti kwani hadi saa sita usiku hakuwa amepokea simu yake yoyote.

Alisema wakati anajiandaa kumpigia mumewe mtoto wake wa mwisho alikuwa amelala lakini ilipokaribia saa saba usiku katika hali isiyotarajia mtoto huyo alikurupuka kutoka usingizini na kuanza kuzungumza maneno yenye ubabiri wa kifo cha baba yake.

Gisela alisema mwanaye huyo alikuwa anasema anamuona baba yake anapigana na watu sita wakiwa na nondo. “Mama naomba mpigie baba yangu niongee naye, mama fanya haraka,” aliniambia mwanangu na kweli nikampigia simu baba yake, simu ikawa haipatikani,” alisema.

Mama huyo aliongeza kuwa hali hiyo ilimtia hofu kwani mtoto huyo hakuishia hapo tu, alianza kupiga kelele chumba kizima akirudia maneno yaleyale na alifika mbali zaidi kwa kumuambia mama yake kuwa watoke nje wakamsaidie baba yake kwani wanataka kumuua.

Mama huyo alisema maneno hayo yalimtia hofu hasa alipoona muda umezidi kwenda na haikuwa kawaida ya mwanaye kukaa macho muda kama huo na kusema maneno hayo, hivyo akaamua kumpigia simu dereva mwenzake wa bodaboda ambaye ni rafiki wa mumewe pale kijiweni, akamuambia kuwa yeye tayari amesharudi kwake na amelala.

Bodaboda huyo alimueleza kuwa mumewe aliondoka majira ya saa sita usiku kijiweni hapo lakini ilionekana kama alikuwa amepigiwa simu na mtu aliyemfahamu hivyo baada ya hapo hakuwa na taarifa naye tena.

Mke huyo wa marehemu alisema usiku huo ulipita bila kupata usingizi na kulipokucha aliwasiliana na jamaa zake pale kijiweni pamoja na kuwataarifu ndugu wa mumewe kutokuonekana kwake. Alisema juhudi za kumtafuta zilianza huku akishirikiana na bodaboda wenzake ambapo walikwenda Kituo cha Polisi Mbezi Kwa Yusuph kwa ajili ya kutoa taarifa na polisi waliwapa baraka zote za kwenda kumtafuta mumewe sehemu zote za jamii lakini kwa siku hiyo waligonga mwamba.

Ushirikiano mkubwa wa watu wa bodaboda hatimaye siku ya pili ulizaa matunda ambapo mmoja wao aliyekuwa ameenda Hospitali ya Muhimbili alifanikiwa kuuona mwili wa marehemu mumewe ukiwa katika hali mbaya na kuelezwa kuwa uliokotwa Coco Beach.

Alisema awali walimficha lakini walimpigia simu na kumueleza arudi tu nyumbani kwani wakati huo yeye alikuwa Hospitali ya Palestina, Sinza. Lakini katika hali ya kushtua alisema aliporudi nyumbani alishuhudia bodaboda wengi wakiwa wamejaa nyumbani kwake wengine wakiwa wamekaa vikao pembeni mwa nyumba yao na aliwasihi wamueleze ukweli, ndipo walipomueleza kuwa mumewe ameuawa.

Alisema walifuata taratibu zote za kipolisi kisha wakapewa mwili na akashuhudia marehemu akiwa na jeraha kubwa shingoni kama mtu aliyekatwa na kamba ama kuchinjwa lakini mbaya zaidi ni jinsi wauaji hao walivyomtoboa macho. Gisela alisema walikwenda kumzika mumewe Moshi mkoani Kilimanjaro na akasema kuuawa kwa mumewe ni pengo kubwa kwake kwani ameachiwa watoto wadogo watatu.

“Nawashukuru bodaboda wote wa kituo cha Mbezi Mwisho, ndugu wa mume wangu kwa ushirikiano mkubwa walionipa kwenye kipindi hiki kigumu,” alisema mama huyo. Gazeti hili lilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, ACP Jumanne Muliro ili azungumzie tukio hilo hakuweza kupatikana.

Stori: Mwandishi Wetu, Amani