×

CMSA YAZINDUA MAFUNZO YA MASOKO YA MITAJI

Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, Nicodemus Mkama,akizungumza na waandishi wa habari. 
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, Emmanuel Kakwezi, naye akizungumza.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Chartered Institute For Securities & Investment, Kevin Moore, akihutubia. 
Baadhi ya wageni waalikwa wakifuatilia hafla hiyo.

 

MAMLAKA ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Mafunzo ya Masoko ya Mitaji na Uwekezaji (CISI) wamezindua mpango wa kuendesha mafunzo endelevu ya kitaaluma kwa washiriki wa masoko ya mitaji nchini.

 

 

Ushirikiano huo ni sehemu ya mkakati ya kuwajengea uwezo na kuimarisha ufanisi kwa watendaji na wataalamu wanaoshiriki katika mitaji ili kufikia viwango vya ubora wa kimataifa.

 

 

Hiyo ni hatua muhimu ya utekelezaji wa itifaki ya Soko la Pamoja ya Afrika Mashariki kupitia ushirikiano wa Mamlaka za Usimamizi wa Masoko ya mitaji za Afrika Mashariki (EASRA).

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo jijini Dar es Salaam,Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, Nicodemus Mkama, amesema,    mpango huo unaweka utaratibu na vigezo vya ushiriki kwa washiriki wa masoko ya mitaji kufikia angalau masaa 10 ya ushiriki wa mafunzo ya masoko ya mitaji kwa mwaka na kuwa hiyo itakuwa kigezo kimojawapo cha utoaji wa leseni ya ushiriki katika masoko ya mitaji ifikapo Januari 2020.

 

Ameongeza kuwa, washiriki wa masoko ya mitaji walio na leseni watatakiwa kufanya mafunzo na kutekeleza mipango inayotambuliwa na CMSA na CISI katika kutekeleza vigezo vya mpango wa mafunzo endelevu na kupewa idhini itakayotolewa kwa taarifa maalumu itayowasilishwa CMSA kwa ajili ya taarifa na kuweka kumbukumbu.

” Mpango wa mafunzo endelevu (CD) utawawezesha watendaji ndani ya masoko ya mitaji kutoa huduma kwa umahiri mkubwa zaidi kwa kuendana na maendeleo yanayotokea katika masoko ya mitaji duniani.” amesema Mkama.

 

 

“Ushirikiano kati ya Mamlaka ya Taasisi ya CISI unayaweka masoko ya mitaji ya Tanzania katika ramani ya masoko ya mitaji ya dunia kwa kuwa na wataalamu wanaokidhi viwango vya kimataifa.

 

 

Hili linatokana ukweli kwamba mpango wa mafunzo endelevu unahusisha kufuatilia kwa ukaribu na kuweka kumbukumbu ya maarifa, ujuzi na uzoefu mbalimbali ambayo mtu anataka katika utendaji kazi ndani ya masoko ya mitaji kwa njia rasmi na zisizo rasmi baada ya kumaliza mafunzo ya awali,” amesema Mkama.

 

Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, Emmanuel Kakwezi, akizungumza kwa niaba ya mwenyekiti wa bodi hiyo ameitaka mamlaka kuhakikisha inakuwa na wataalamu wa kutosha katika masoko ya mitaji wanajiunga na mpango huo ili kulinda uwezo wa kitaaluma na uhalali wao katika ulimwengu wa ushindani.

 

Amesema, masoko ya mitaji ni sekta inayobadilika kwa kasi na yenye kuhusisha viashiria vya aina mbalimbali.

 

Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya Chartered Institute for Securities & Investment, Kevin Moore, amesema kuwa ushirikiano huo utawawezesha watanzania kuongeza uwezo na ufanisi katika soko la kimataifa.