
DAR ES SALAAM: TUKIO la ndugu wa marehemu Salum Kindamba kususia maiti katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili hadi Jeshi la Polisi litakapomsafisha marehemu kwa tuhuma za ujambazi linaendelea kuzua utata.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, ACP Emmanuel Lukula alisema tukio lilitokea Jumamosi ya Agosti 11 mwaka huu baada ya mtu mmoja kutoa taarifa Polisi kuwa kuna majambazi wanne kwenye Mgahawa wa Clouds Motel na wana mfuko mwekundu wenye bastola.
Hivyo, Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ikashirikiana na mikoa yote ya kipolisi ya kanda kuchukua hatua, hata hivyo, mama, mke, ndugu na rafiki wa marehemu wamesisitiza kuwa Salum hakuwa jambazi.
UWAZI MTAA KWA MTAA
Wakati Jeshi la Polisi na ndugu wa marehemu wakivutana kuhusu tukio hilo gazeti hili baada ya kuonana na ndugu wa marehemu lilipita mtaa kwa mtaa kufuatilia sakata hilo na Alhamisi lilifika katika Mgahawa wa Clouds Motel uliopo katika Mtaa wa Kigilagila, Ilala jijini Dar es Salaam ambako inadaiwa tukio la kukamatwa kwa Salum Kindamba na wenzake Omary Mhando, Agape Kalembo na baadaye Salum kupigwa risasi na kupoteza maisha lilipoanzia.
Wakizungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa majina viongozi na wafanyakazi wa mgahawa huo alilielezea tukio hilo kwa masikitiko.
”Cha ajabu baada ya tukio kutokea hakufika mwandishi yeyote. Tumezoea kuona waandishi wakifika eneo la tukio punde tu baada ya tukio. Tangu Agosti 11 mwaka huu tukio lilipotokea hadi leo hakuna chombo chochote cha habari kilichofika hapa Clouds Motel kupata mwanzo wa habari hii zaidi yako ambaye umefika leo.
“Tunaona habari zinaripotiwa tu kwenye vyombo vya habari na kwenye mitandaoni ya kijamii zikijikita zaidi kwa ndugu na Jeshi la Polisi,” alisema ofisa mmoja wa hoteli hiyo aliyeomba jina lake kutoandikwa gazetini kwa kuwa siyo msemaji. Alisema marehemu na wenzake walikuwa ni wateja katika mgahawa huo na walikuwa wakifika mgahawani hapo mara mojamoja kwa ajili ya kupata chakula.
Uwazi lilipotaka kujua kuhusu namna ya ukamatwaji na mfuko mwekundu uliodaiwa kuwa na bastola, pesa na vitu vingine vilivyotajwa na Jeshi la Polisi walivyokutwa navyo watuhumiwa, ofisa huyo wa mgahawa huo alisema, “Hivyo sivifahamu hebu huyu (jina tunalihifadhi) akujibu kwani yeye ndiye siku ile aliyewahudumia.”
Naye afisa mwingine huyo amelieleza Uwazi kuwa siku hiyo yeye na mwenzake hawakuona mfuko mwekundu, bastola, pesa, simu yenye rangi ya dhahabu ama vitu hivyo vingine vilivyotajwa wakati walipokamatwa watuhumiwa na wakati wanatoka mgahawani.
“Hata askari waliporejea kuchukua magari yaliyoachwa na watuhumiwa hatukuviona hivyo ndani ya gari kwani magari hayo tulikabidhiana hapa mgahawani,” alisema afisa huyo.
Kuhusu kupigwa risasi kwa Salum, afisa huyo alisema: “Hakupigiwa risasi hapa mgahawani! Kama kulikuwa na mazungumzo kati yao sisi hatukuyasikia na hapakuwa na purukushani yoyote iliyotokea hapa. Walipowekwa chini ya ulinzi walitii amri bila shuruti wakatoka nao nje.”
Alisema marehemu na wenzake walifika mgahawani siku hiyo wakiwa katika makundi mawili. Kwanza walifika wawili wakaegesha gari walilokuwa nalo nje, wakaketi mezani na kuagiza chakula, baadaye wengine wawili walifika na gari lingine wakaliegesha nje, wakajiunga katika ile meza ya wenzao.
“Punde waliingia watu wawili, mmoja mwanamke na mwingine mwanaume wakaketi meza iliyokuwa karibu na akina Salum.
“Tulichoshuhudia ni wale jamaa wawili walioingia baada ya akina Salum kujitambulisha wao kuwa ni askari Polisi. Wakatueleza kuwa akina Salum ni watuhumiwa wa ujambazi hivyo wako chini ya ulinzi, wakatoka nao nje. Hapa kwetu yalibaki magari tu ya watuhumiwa ambayo nayo Polisi waliyafuata, tukayakabidhi na ndipo tulipotaarifiwa kifo cha mmoja wao,” alisema.
Gazeti hili lilihoji shuhuda wa tukio hilo ambaye siku ya tukio alikuwa pembeni mwa Clouds Motel ambaye hakutaka kutajwa jina lake. Amesema, “Sijui sababu ni nini ila wote walitolewa humo mgahawani. Mmoja wa watuhumiwa alielekea nyuma na askari akamfuata ndipo baadaye tukapata taarifa kuwa jitihada za kumkamata zilishindikana ikawa ndivyo hivyo tena.”
Uwazi halikuishia hapo lilifika kazini kwa marehemu Salum Kindamba kwenye Kiwanda cha Alaf ambapo jitihada za kuzungumza na afisa mwajiri ziligonga mwamba na wafanyakazi wa kiwanda wakiwemo walinzi walimtaja kuwa ndiye msemaji rasmi wa kiwanda.
Baada ya kuruhusiwa kuingia kiwandani mwana mama mmoja aliyedaiwa kuwa ndiye msemaji rasmi wa Alaf bila hata kujitambulisha jina alipoonana na mwandishi wetu alisema: “Sikutani na mtu isipokuwa tu kama ana ahadi na mimi. Pia kuhusu hayo maswali yako kama unahitaji majibu nenda kaandike barua Jumatatu ilete. Tutakujibu kwa barua.”
Hata hivyo, baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda hicho wamesema, kazi ya marehemu Salum kiwandani hapo ilikuwa ni kuendesha mitambo inayozalisha bidhaa za Alaf na tangu aanze kazi kiwandani wao hawajasikia tukio lolote la ajabu na Jumamosi ya Agosti 11 siku aliyouawa alifika kazini. “Mnazungumzia Salum peke yake! Mbona wote wanne ni wafanyakazi wa hapa Alaf,” alidai mmoja wa wafanyakazi kiwandani hapo.
Gazeti hili lifika ofisini kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, ACP Emmanuel Lukula na kukutana na askari aliyejitambulisha kwa jina la Afande Steve; alipotaka kujua anachokitaka mwandishi aliambiwa ni kuhusu marehemu Salum na kama ndani ya mfuko mwekundu bastola ilipatikana wakati wanawatia nguvuni watuhumiwa.
“Kamanda Lukula ametoka muda si mrefu na sijui kama atarejea ofisini ama hatarejea, ndiye angejibu maswali yako hayo. Isitoshe leo ni wikiendi,” alisema askari huyo. Kamanda Lukula alipopigiwa simu mara kadhaa hakuweza kupatikana.
STORI: DENIS PATRICK, UWAZI