×

OFM YAMNASA DARASA

Shariff Thabeet ‘DarassaDAR ES SALAAM: Baada ya Kikosi Fichua Maovu (OFM) kutumia muda mrefu kumsaka, hatimaye msanii wa Bongo Fleva aliyewahi kutamba na Wimbo wa Muziki, Shariff Thabeet ‘Darassa’ amenaswa mjengoni kwake jijini Dar.

Kwa muda sasa, kumekuwa na taarifa tofauti juu ya msanii huyo kupotea kwenye muziki huku madai yakielekezwa kuwa ametopea kwenye matumizi ya dawa za kulevya.

Licha ya kumtafuta sehemu nyingi ikiwemo kituo cha kuhudumia waathirika wa dawa za kulevya ‘Sober’ za Bagamoyo, Kigamboni, Iringa na Zanzibar, wiki chache zilizopita baada ya gazeti hili kutoka na habari ukurasa wa mbele iliosomeka; Madai ya kubwia unga…NDUGU WA DARASSA WAVUNJA UKIMYA, OFM lilipigiwa simu na Darassa mwenyewe na kuelekezwa hadi eneo analoishi ambalo lipo nje kidogo ya Jiji la Dar.

OFM kama ilivyo jina lake, lilifika eneo hilo analoishi ambapo lilikutana moja kwa moja na Darassa mwenyewe akiwa amembebelea mtoto wake wa kike huku hali yake kiafya ikiwa safi tofauti na inavyoenezwa. “Huyu ndiye mwanangu, maneno yamesemwa sana lakini huyu ndiye aliyenifanya kukaa chini kwa muda na kulea,” alisema Darassa huku akimbembeleza mwanaye huyo mwenye miezi kadhaa.

Mara baada ya kumtambulisha mwanaye, Darassa aliwatembeza OFM katika mjengo wake wa kifahari. “Hii hapa ni studio yangu, maisha yangu yote yapo hapa, huwezi kunikuta nikitamba studio yoyote, vitu vyote napikia hapa,” alisema Darassa.

Pamoja na kujionea mjengo wa kifahari, OFM pia ilipata kutupia jicho kwenye magari yake ya kifahari yaliokuwa yamezunguka neo hilo yakiwemo BMW pamoja na Toyota Alphard.

STORI: Waandishi Wetu, Ijumaa