MBUMGE wa Kawe kwa tiketi ya Chadema, Halima James Mdee amedai kwamba taratibu zilizotumika kuibadilisha manispaa ya Dodoma kuwa Jiji la Dodoma hazikufata taratibu kisheria kwa sababu hazikupitia Bungeni kuidhinishwa na bunge hilo.
September 4, 2018 Wabunge walikuwa wakijadili Muswada wa sheria ya kulitangaza jiji la Dodoma kuwa makao makuu ya nchi wa mwaka 2018 (The Dodoma capital city Declaration Bill 2018) ambapo miongoni mwa waliopata nafasi ya kuchangia ni pamoja na Mbunge wa Kawe Halima Mdee ambaye amekosoa taratibu zilizotumika na Serikali katika kutekeleza mapendekezo hayo.
“Isije ikajengwa propaganda kwamba kuna mtu anapinga Dodoma kuwa makao makuu maana sasa hivi siasa zetu zimetoka katika hoja na kwenda katika vihoja, Mimi nimekuwa mbunge kwa awamu tatu, mara ya kwanza nikiwa mbunge wa viti maalum na kisha mbunge wa jimbo kwa mara mbili, sijawahi kuona Bunge linalopelekwa pelekwa kama hili. Sasa mtuambie ni lini Bunge hili lililetewa muswada wa sheria ambao uliinyanyua Dodoma kuwa jiji,” amesema.
Aidha, amedai kwamba serikali ilikuwa haijajipanga kuipa jiji la Dodoma kwa sababu hata ofisi zilikuwa hazijajengwa jambo lililopelekea kuteuliwa kwa baadhi ya majengo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) yatumike kama jambo ambalo amedai linaweza kusababisha mabinti wa chuo hicho wakajikutawanaingia kwenye ushawishi wa kimahusiano hatimaye ujauzito.