
KLABU ya Simba leo Jumamosi inatarajia kucheza mchezo wa kirafiki na AFC Leopards ya Kenya kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mechi hiyo iliyopangwa kuanza saa 12 jioni, imeombwa makusudi na Kocha Mkuu wa timu hiyo Mbelgiji, Patrick Aussems kwa ajili ya kuwapa nafasi ya kucheza wachezaji wanaoanzia benchi katika kikosi chake.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara alisema wanacheza
mechi hiyo ya kirafiki kwa ajili ya kuwaweka fiti wachezaji wao baada ya Ligi Kuu Bara kusimama kupisha mechi za timu za taifa za kufuzu Afcon.

“Kocha aliomba apate japo mechi moja katika kipindi hiki na sisi tumesikiliza mawazo yake Hivyo tumeamua kuwaita AFC Leopards kutoka Kenya kwa sababu tumekuwa tukicheza nao mara nyingi na wao hawakukataa, wameitikia ombi letu,” alisema Manara.
Kwa upande wa Kocha Msaidizi wa Leopards, Thomas Juma, alisema kuwa: “Nimefurahi kucheza na Simba kwa mara nyingine tena, naamini tutashinda mchezo huu ingawa siyo rahisi kwa sababu Simba ni timu kubwa.”