×

WACHUNGAJI WAANGUSHA MAOMBI ALIPOFIA MTIKILA

PWANI: Wachungaji wawili; Steven Shengo, John Kidobi na mke wa aliyekuwa mwanasiasa machachari hapa nchini, na Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party ‘DP’, Hayati Christopher Mtikila, Georgia Mtikila (pichani), Jumapili iliyopita walivamia eneo alilopatia ajali na kufariki dunia mumewe huyo.  

 

Mke wa Mtikila na wachungaji hao walifika eneo hilo baada ya kupewa taarifa kwamba watu wabaya wanalitumia kufanya mambo ya kishirikina. Baada ya kufika eneo la tukio katika Kijiji cha Kibiki, Chalinze mkoani Pwani waliangusha maombi mazito na kukemea vikali ushirikina unaofanya katika eneo hilo.

 

Wanahabari ambao baada kusikia taarifa za msafara huo nao walifika eneo hilo na kuwakuta wachungaji hao wakiangusha maombi ya nguvu sehemu hiyo inayosemekana kuwa na mauzauza ya kutisha hasa nyakati za usiku. Miongoni mwa mauzauza yanayoendelea katika eneo hilo ni sehemu ambayo inasemekana kuna mtu huwa anaota moto usiku eneo hilo.

 

Alipohojiwa na gazeti hili mama Mtikila alisema alishapata taarifa za mtu huyo kuonekana usiku hapo lakini shauku yake kubwa kufika eneo hilo ambalo alikuwa hajawahi kufika tangu kifo kutokea ilikuwa ni kupaona mahali hapo anapootaga moto mtu huyo. Akiwa eneo hilo mama Mtikila alijionea majivu mapya yaliyoonesha ukweli kuwa hata siku hiyo usiku wake mtu huyo anayedaiwa kuota moto alikuwepo.

 

“Jamaaniii kumbe ni kweli taarifa za mtu anayeotaga moto kwenye eneo alilofia mume wangu…Haya majivu yanaonesha kabisa huu moto ni wa usiku wa kuamkia leo,” alisema mama Mtikila huku akibubujikwa na machozi. Sambamba na mtu huyo mama huyo alishangaa kuona tuta mfano wa kaburi likiwa limewekewa miti kwenye kila kona ambapo mama huyo alianza kuing’oa huku akifanya maombi kwa kushirikiana na wachungaji aliofuatana nao.

Mauzauza mengine yalimchanganya mama Mtikila ni mawe yaliyopangwa kwa staili ya mnara na vikorokoro vingine vinavyoonesha kuwa mahali hapo kuna kazi kubwa ambayo huenda huwa inafanyika usiku. Kitu kingine ambacho kilimtoa machozi mama huyo ni mabaki ya gari alilopata nalo ajali mumewe ambayo yamebandikwa kwenye mti ambao gari liliugonga na kumsababishia umauti Oktoba 4, 2015.

 

Mama huyo alizidi kuangusha maombi makali huku akizunguka eneo hilo lililokuwa na majani marefu. Akizungumza na wanahabari wetu, mama Mtikila alisema dhumuni la safari yake ya kulitembelea eneo hilo ni baada ya kumkumbuka mumewe huyo lakini pia kuthibitisha madai ya kuonekana mauzauza katika eneo hilo.

 

Baada ya kutoka eneo hilo mama Mtikila na wachungaji aliokuwa nao walimtafuta Kamanda wa Ulinzi Shirikishi Kata ya Chalinze, aliyefahamika kwa jina la Puto ambaye naye alimueleza changamoto zilizopo eneo hilo. “Ni kweli kuna mauzauza na kuna mtu huwa anaota moto usiku pale alipofia Mchungaji Mtikila,” alisema kamanda huyo.

Stori: Richard Bukos, Amani