
SIKU chache baada ya kuonyesha uwezo mzuri na kufunga mabao mawili katika timu ya taifa ya England, mshambuliaji Marcus Rashford ametolewa kauli ambayo inaweza kutishia uwepo wake ndani ya Manchester United.
Kocha wa England, Gareth Southgate amemtumia chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 20 katika michezo mwili iliyopita dhidi ya Hispania na Uswisi na kutoa tamko kuwa hatawachagua wachezaji ambao hawapati nafasi katika klabu zao.
Kauli hiyo inaweza kumtikisa Rashford kwa kuwa hana uhakika wa kucheza katika kikosi cha kwanza cha klabu yake.
“Wachezaji ambao hawapati nafasi ya kucheza kwenye klabu zao hatutakuwa na nafasi kwao, wanapocheza klabuni wanakuwa fiti na inaboresha viwango vyao.
“Marcus ana changamoto kubwa ya nafasi katika klabu yake, siyo kazi yangu kuingilia majukumu ya kocha, wana kikosi kipana na michuano mingi lakini naamini Jose (Mourinho) anajua kuhusu ulimwengu aliopo Marcus.
“Anamkubali lakini Marcus hajapata nafasi ya kucheza mechi nyingi, nimefurahi ameondoka kambini akiwa na hali ya kujiamini kwa kiwango cha juu,” alisema kocha huyo.
Kauli hiyo pia inaweza kuwa mwiba kwa mshambuliaji Danny Welbeck wa Arsenal ambaye amekuwa na nafasi ngumu ya kucheza kikosini kwake.