The House of Favourite Newspapers

Ajibu Aamua Kujitoa Muhanga Yanga

 

Ibrahim Ajibu

STRAIKA mwenye asisti za kumwaga ndani ya Yanga, Ibrahim Ajibu amewa­sisitiza mashabiki wa klabu hiyo kuwaunga mkono kama ilivyokuwa kwenye mechi na Simba lakini yeye atapambana kibabe zaidi.

 

“Kwa sasa Yanga ndiyo nyumbani kwetu kwa hiyo nataka kuona msimu huu tunafanya vizuri lakini pia kuendeleza rekodi yetu ya kutofungwa ambayo tunaishika mpaka sasa.

 

“Lakini pia niwaombe tu Wanayanga wote kuwa kitu kimoja kuanzia sasa na wasiruhusu mgogoro wowote ule ambao unaweza kukwamisha malengo yetu hayo,” alisema Ajibu na kuongeza kuwa Mbao analala kilaini leo Uwanja wa Taifa.

Awekewa kikao nyumbani

Athumani Ajibu ambaye ni kaka mkubwa wa Ibrahim Ajibu amesema kuwa wameamua kukaa chini na mchezaji huyo ili aweze kutambua thamani yake akiwa uwanjani na nje ya uwanja kwa kuwa anapaswa afanye mambo makubwa zaidi ya aliyoyafanya.

 

“Unajua msimu uliopita Ajibu hakuwa katika ubora wake hivyo tulichoamua kufanya msimu huu tulikaa naye chini na tukamwambia kwamba athamini kazi yake ya mpira kwa kutumia vema kipaji chake alichopewa na Mungu.

 

“Bado hatujaridhishwa na kiwango anachoonesha kwa kuwa tunatambua ana kipaji kikubwa hivyo kwa kuwa ametusikiliza na ametuahidi atabadilika hivyo tunaamini tutashuhudia makubwa msimu huu,” alisema Athumani.

Comments are closed.