×

Mkongo Yanga Agomea Namba Ya Fei Toto

Feisal Salum ‘Fei Toto’ (wa tatu kutoka kulia).

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema kamwe hawezi kumbadilisha namba kiungo wake mkabaji, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na kumpeleka kwenye ushambuliaji kama ambavyo alicheza hivi karibuni kwenye mechi ya timu ya Tanzania, Taifa Stars.

Zahera amekuwa akimtumia Fei Toto kama kiungo mkabaji kwenye michezo yote sita ambayo alianza kwenye kikosi hicho lakini kwenye mechi ya Stars dhidi ya Cape Verde chini ya Kocha Emmanuel Amunike, kiungo huyo alicheza kama kiungo mshambuliaji.

Mwinyi Zahera.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Zahera amesema kwamba kwake anapenda zaidi kumtumia kiungo huyo kwenye eneo hilo la ukabaji na ataendelea kumchezesha hapo kwenye michezo yao ijayo ya Ligi Kuu Bara.

 

“Watu hawajui kama kwenye mpira hakuna tofauti ya namba sita na nane. Wote wanacheza katikati ya uwanja mmoja kulia na mwingine kushoto.

 

“Tofauti yao inakuja pale ambapo wanapewa majukumu ya kufanya uwanjani, kama timu inashambulia mmoja atasogea juu na mwingine atabaki kwa ajili ya kulinda walinzi.

 

“Kwangu mimi hizo nafasi hazina maana yoyote ile bali natazama zaidi timu ambavyo inacheza, siwezi kubadili kitu kwa sasa nitaendelea kutumia kama tulivyocheza awali,” alisema Zahera.

Stori na Said Ally